POLISI Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, imewakamata watu 11, kwa tuhuma za wizi wa nyaya za umeme zilizoko katika nguzo za taa za barabarani, maeneo tofauti ndani ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna wa Polisi Msaidizi, Awadhi Juma Haji, alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada jeshi hilo kupokea taarifa za uwepo wa vitendo hivyo na kuweka mtego.
Alieleza kuwa katika tukio la kwanza, Julai 26, mwaka huu, saa 8:00 usiku, eneo la Saaateni, Wilaya ya Mjini, barabara kuu ya kutoka Bububu/Mjini, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne, huku wengine wakifanikiwa kukimbia, wakiwa wanaiba nyaya za umeme katika nguzo za taa za barabarani zilizopo eneo hilo.
Aliwataja watuhumiwa hao ni Mohamed Shaamte Mohammed (16), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Mwembeladu, Salum Khamis Ibrahim (18), mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya High Perfomance, Mohammed Khamis Ali (27), mkazi wa Mwembemakumbi na Makame Khamis Ali (19), mkazi wa Chumbuni.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na waya wenye urefu wa mita 34, waliouiba katika nguzo 8/282 na mwingine waliouiba nguzo namba 7/265, kwa kutumia visu viwili vikubwa.
Katika tukio lingine, Kamanda huyo alisema Julai 29, mwaka huu, saa 8:30 usiku, maeneo ya Kibweni, karibu na makao makuu ya kikosi cha KMKM, waliwakamata watuhumiwa wawili, waliofanikiwa kukata waya katika nguzo namba 4/119 na 4/120, barabara kuu ya kutoka Bububu Mjini.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Ali Juma (23) na Fadhili Ali Juma (19), wote wavuvi na wakazi wa Mahonda, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Unguja, ambao walikutwa wakiwa na visu viwili vya kufanyia uhalifu huo.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, watuhumiwa hao baada ya kukamatwa, waliwataja watu wanaowapelekea kuwauzia nyaya hizo, ambao ni wafanyabiashara wa vyuma chakavu, ambao huwauzia kwa kilo moja kwa sh. 5,000.
Alisema baada ya watuhumiwa hao kutaja sehemu wanapofanya biashara hiyo, polisi walifanikiwa kufika mpaka katika ghala hilo, ambako waliwatia mbaroni watu watano, wanaojihusisha na ununuzi wa nyaya hizo na kufanikiwa kukamata kilogramu 4,720, za nyaya kutoka kwa watuhumiwa hao.
Kamanda huyo aliwataja wanaonunua nyaya hizo kuwa ni Ajuwedi Juma Ajuwedi (30), mkazi wa Mwera, ambaye alikamatwa akiwa na kilogramu 82 za nyaya, Ramadhan Riziki Abdallah (36), mkazi wa Amani, aliyekutwa na kilogramu 26.
“Kati ya watuhumiwa hao, watatu waliokuwepo katika ghala la kampuni ya Zanzibar Steel CO.LTD, lililoko eneo la kwa Mchina, Wilaya ya Magharibi B, walikutwa wakiwa na kilogramu 4,613m za nyaya hizo,” alisema.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mikidadi Hamdu (48), mkazi wa Mpendae, ambaye ni mmiliki wa ghala hilo, meneja wa ghala, Rida Khalifeh Hussein (28), mkazi wa Mbweni na msimamizi wa ghala, Amin Said Saleh (38), mkazi wa Tomondo.
Haji alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na upelelezi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani. Aliongeza kuwa jitihada za kuwatafuta wote waliotajwa kujihusisha na vitendo hivyo bado zinaendelea.
Aliwaonya wote wanaohujumu miundombinu ya umeme, kuacha mara moja.