UJENZI wa bandari ya Karema ya kimkakati inayoendelea kujengwa katika wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi itakayotumika kwa ajili ya kusafirishia mizingo na abilia kutoka Tanzania kwenda nchi ya DRC Congo baada ya kukamilika, Ujenzi huo umeanza kuhujumiwa kwa kufanyika wizi wa vifaa mbalimbali.
Uhujumi huo umebainika baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kufanya operesheni ya misako maalumu ya kudhibiti mtandao wa wizi wa rasilimali za mradi huo na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 16 wakiwa wameiba mafuta ya diseli lita 4,100 na nondo 68 na vifaa mbalimbali mali ya kampuni inayojenga bandari hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika Vijiji vya Karema na Ikola kufuatia msako makali uliofanywa na jeshi hilo.
Amesema kabla ya kufanyika kwa msako huo Jeshi la Polisi walipata taarifa juu ya hujuma za wizi kwenye ujenzi huo unayotarajiwa kukamilika Machi 6, 2022.
Baada ya taalifa hizo kufika kwa jeshi la polisi walifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 16 wakiwa na mafuta aina ya diseli lita 4,100, vipande 58 vya nondo , madumu 118 ya plasitiki, betri mbili za gari, grisi kilo saba na oili lita 10 vyote vikiwa mali ya Kampuni ya XIAMEN ON COING CONSTRACTION GROUP COMPANY LIMETED inayotekeleza mradi huo.
Kamanda Kuzaga amewataja watuhumiwa hao waliokamatwa kuwa ni Jackson Mathias Mkazi wa Ikola ,Godfey Kigongo, Joseph Haule wakazi wa Kijiji cha Karema, Ibrahimu Simba Mkazi wa Kijiji cha Inyonga , Ayubu Athuman, Chuki Wiliam, Jipala Nekala , Lusonguye Kaise , Jacob Thobias Muse Enelil Benedictor wote wakazi wa Karema .
Ameeleza kuwa, watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na matukio hayo ya wizi na baada ya taratibu zote za kiupelelezi kukamilika jalada litafikishwa katika ofisi ya Taifa ya mashitaka Mkoa wa Katavi kwa hatua zaidi za kisheria .
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewaagiza watu wote ambao wamehusika na wizi katika Bandari hiyo, wajisalimishe kabla hawaja kamatwa kwani endapo watashindwa kusalimisha mali walizoiba wakikamatwa watachukuliwa hatua kali ikiwemo kuwekwa mahabusu bila kutoka kwani kosa hilo lina husiana na kuhujumu uchumi.

RC Mrindoko amebainisha kuwa, kitendo hicho cha wizi ni aibu kwani mradi huo umewekwa kwa ajiri ya kuwasaidia, badala yake wao ndio wamekuwa watu wanaofanya uhalifu.
Na George Mwigulu,Katavi