NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallaha Ulega, amewasisitiza viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha ulinzi unakuwepo kwa wawekezaji wa vizimba vya kufugia samaki .
Naibu Waziri Ulega ameyasema hayo wakati wa Ziara yake alipotembelea na kukagua vizimba 24 vya samaki vya Kampuni ya TanGreen Aqual vilivyopo Wilayani Magu, Mkoani Mwanza, ili kuboresha na kulinda uwekezaji wa uchumi wa buluu.
Ulega amesema kuwa wawekezaji wanaokuja kuwekeza chini ni vyema wakalindwa kwani kazi ya kuwekeza pesa ni ya utayari hivyo kamati ya ulinzi na usalama ni jukumu lao kuhakikisha wanawalindwa kwani kumekuwa na watanzania baadhi wenye tabia za udokozi.
‘’Serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi imetenga fedha katika bajeti ya 2021, 2022 ambayo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili yakutenga maeneo mahususi ya kufanyia shughuli za uvuvi wa vizimba na uvuvi wa asili ili kuleta tija katika kuwekeza katika Uchumi wa buluu na kulinda uwekezaji unaofanyika ziwani” amesema

Katibu MKuu Uvuvu, Rashid Tamatama ameongeza kuwa wizara ipo kwenye juhudi za kuvutia wawekezaji wa uvuvu kwa njia ya vizimba ili kuongeza uzalishaji wa samaki kufikia tani 50 kwa mwaka.
‘’katika miaka minne iliyopita kulikuwa na vizimba visivyozidi 20 nchin, sasa hivi kuna vizimba zaidi ya 473 na muwekezaji huyu TanGreen Aqual ltd kwa sasa ndio anaongoza kwa kanda ya Ziwa kwani atakuwa na uwezo wakuzalisha samaki tani 10,000 kwa Mwaka’’ amesema Tamatama
Aidha, katika kuendelea kupunguza changamoto ya Vifaranga vya samaki Tamatama amesema serikali imetoa Tsh. 5.9 bilioni kwa ajili yakuzalisha vifaranga vya samaki
Daktari wakutibu samaki katika eneo hilo la uwekezaji ,Mugure Mariwanda, amesema mradi huo umegharimu Tsh 4.6 bilioni na unatarajia kuongeza maeneo ya uzalishaji wa samaki na kufikia kuwa na mabwawa 100 na vizimba 1200 vya kufugia samaki ifikapo 2022.
Amesema changamoto inayokabili mradi ni upatikanaji wa vifaranga vya samaki nchini, na pia kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wavuvi kuingia ndani ya eneo la mradi na kuiba pamoja na kuharibu miundombinu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Magu, Kiswaga Destery, amesema wananchi wa wilaya hiyo watanufaika na uchumi wa buluu unaofanywa sasa kwani wawekezaji wengi sasa wanakuja kuwekeza ufugaji wa vizimba
‘’tumepokea maelekezo ya kuimarisha ulinzi kwa wawekezaji katika wilaya yetu ili tija ionekane kwa wawekezaji na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salimu Kali, amesema muwekezaji huyo TanGreen Aqual amefuata utaratibu zote za uwekezaji katika kata hiyo ya Kitongosima ulipo mradi huo.
Na Johari Shani, MWANZA