WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso, amesema serikali ipo mbioni kuanzisha mita za kulipia maji kadiri unavyotumia, ili kuondoa ubadhirifu katika usomaji wa mita hizo.
Amesema usomaji mita za maji umekuwa na malalamiko kwa wananchi wengi wakilalamikia kubambikiwa ankara, tofauti na matumizi yao ya kila siku.
Kutokana na hilo, mita hizo zitamfanya mteja kulipia ankara kwa kadiri anavyotumia kiwango cha maji kama ilivyo kwenye umeme ambapo watumiaji wa umeme wanalipa Ankara zao kwa mfumo wa luku.
Akizungumza Dar es Salaam, katika utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wa maji wa mshikamano, wilayani Ubungo, Waziri Aweso alisema uwekaji wa mita za ‘LUKU’ utapunguza malalamiko na changamoto kwa wananchi.
“Mwananchi atanunua maji kulingana na uwezo wake, kama akitoa sh. 10,000 atapata maji ya gharama hiyo na akitoa 100,000 atapata maji ya gharama hiyo, lakini isiwe anabambikiwa bili ovyo ovyo,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Aweso alisisitiza katika suala la mita hizo, hatataka kuona mtu au watu wanahujumu miundombinu hiyo. MAELEKEZO MUHIMU DAWA Katika utiaji saini huo, Waziri aweso alitoa maelekezo kwa DAWASA kuwa, wasoma mita za maji wawe waangalifu kwa kuwashirikisha wananchi katika usomaji wao na wasitumie muda mrefu kuwaunganishia maji wananchi.
Alisema siku 14 zinatosha kuunganisha huduma hiyo na kuwataka viongozi wa DAWASA kupitia gharama za maunganisho, ili kusitokee manung’uniko kwa wateja. Pia, katika mkutano huo, Aweso alipongeza kazi nzuri inayofanywa na bodi ya DAWASA katika utekeleza majukumu yake ili kutimiza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kumtua ndoo mwanamke.
“Najua kila kukicha, nyumba na wakazi wanaongezeka mkoa wa Dar es Salaam, lakini serikali inadhamira moja tu ya kumtua ndoo mwanamke,” alisema.
Akizungumzia kuhusu uhaba wa maji katika Jimbo la Kibamba, alisema Mbunge wa jimbo hilo, Abbas Mtevu, amekuwa akifanya jitahada kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi.
“Jitihada za mbunge huyu zinasikika kwasababu anaziongelea ndani ya Bunge, hivyo serikali itahakikisha Kibamba yote inapata maji safi na salama,” alisema. MAENEO
YATAKAYONUFAIKA
Waziri Aweso alitaja maeneo yatakayofaidika na mradi huo ni Luguruni lapaz, Mbezi Inn, Magari saba, Magayana, Njiapanda Makondeni, TAKUKURU, Kwa Gamba, Luguruni Dampo na Luguruni KKKT.
Maeneo mengine ni, Rising Star, Msakuzi Supermarket, Machimbo, Amani Street, Miti Mirefu, Madafu, Kwa Mfala, Chikongowe, Masaki Street, Msakuzi Kusini, Msakuzi Kaskazini, Makabe, Mbezi Luisi, Kwa Robert, Mageti, Mbezi Msumi Mpiji Magohe na Machimbo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema mamlaka hiyo inahudumia majimbo 16 ya uchaguzi, mojawapo likiwa Kibamba.
Alisema huduma ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaam imetekelezwa kwa asilimia 92 na asilimia nane zipo Kibamba ingawa zimechelewa.
Alieleza kuwa, serikali imekusudia kuondoa changamoto ya maji katika Jimbo la Kibamba ndani ya muda mfupi, jitihada hizo zinafanyika kwasababu ya ufatiliaji wa mbunge huyo.
Alisema akishirikiana na timu yake ya DAWASA, anakusudia Kibamba ipate maji kwa asilimia 100 siku chache zijazo, ili kumuunga mkono Mtevu na serikali kwa ujumla.
Alisema sasa Kibamba ina miradi mitano ya maji, ukiwemo huo ambao unahusisha ujenzi wa tanki la maji Mshikamano, ujenzi wa pampu nne za kusukuma maji na kisima vyote vikiwa na thamani ya sh. bilioni 5.4 ambayo inatokana mapato ya DAWASA.
Alisema mradi wa pili ambao unatekelezwa ndani ya jimbo hilo una thamani ya sh. bilioni 65 na kwamba sehemu ya mradi huo, imegusa maeneo ya Kibamba ukianzia Changanyikeni hadi Bagamoyo.
Alitaja maeneo yatakayonufaika na mradi huo ni Goba, kibururu Chaurembo, Njianane, Uzaramuni, Muungano, Matosa, Matosa Mbuyuni, Tegeta A, Kulangwa Kinzudi na Mbezi. Alisema mradi huo ni mkubwa ambao umehusisha kilomita 1026 na hadi sasa kilomita 580 zimekamilika na matanki matatu yamekamilika ambapo tanki la Tegeta A limefikia asilimia 90 ya ujenzi wake, Vikawe limekamilika na tanki la Mbezi likifikia asilimia 80.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia watu zaidi ya 100,000. BODI YA DAWASA Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Kate Kamba aliipongeza DAWASA kwa ufanisi wa kuwaondolea changamoto ya maji wananchi wa Dar es Salaam.
“Naipongeza DAWASA kwa kufanya kazi kwa vitendo ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema Kate.