POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam imewakamata watu 17 kwa tuhuma za kuuza jezi bandia 1208 za timu ya Yanga zinazotengenezwa na kusambazwa na kampuni ya GSM.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo,Jumanne Muliro amesema jezi hizo zimekamatwa baada ya polisi kufanya ufuatiliaji kuanzia Januari 2 hadi 28 mwaka huu.
Kamanda Muliro amesema polisi walifanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na baadhi ya mikoa nchini na kuzibaini jumla ya jezi bandia 1208.
“Kwa Dar es Salaam, watuhumiwa watano wamekamatwa ambao ni Zahiri Hassan ambaye alikutwa na jezi 52 katika Uwanja Benjamin William Mkapa na eneo la Kariakoo mtaa wa Agrey alikamatwa Majiba Ndahya akiwa na Jezi 124,” amesema
Amewataja watuhumiwa wengine ni Mohamed Ramadhani akiwa na jezi feki 86,John Staslaus (39) na Emmanuel Kinasa Jezi 60.
Amesema baada ya kuwahoji watuhumiwa hao waliwataja wenzao ambao wapo Zanzibar ambapo katika Uwanja wa Amani jumla ya watuhumiwa watatu walikutwa na Jezi bandia 36.
“Jezi zingine bandia 134 zilipatikana kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Tanga na mkoa wa Mwanza watuhumiwa tisa walikutwa na Jezi 811,” amesema.
Kamanda Muliro amewaonya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya kutengeneza, kuuza na kusambaza bidhaa kwa kuiga au kufananisha nembo za biashara kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria.
“Ninawatahadharisha wananchi wanaojihusisha na vitendo vya kutengeneza, kuuza na kusambaza,bidhaa kwa kuiga au kufananisha nembo za biashara au huduma za watu wengine iliyosajiliwa kisheria, kufanya hivyo ni kosa na kinyume cha sheria za nchi,”amesema.
Hata hivyo Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam imeahidi kushirikiana na mamlaka nyingine za kisheria ili kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Na ATHNATH MKIRAMWENI