SERIKALI ya Ujerumani imeipatia Tanzania msaada mwingine wa Euro milioni 45 sawa na sh. bilioni 119.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu katika sekta za maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Msaada huo umekuja siku mbili tangu nchi hiyo iingie makubaliano mengine ya kutoa msaada wa Euro milioni 71 sawa na zaidi ya sh. bilioni 190.5, kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, afya ya mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza jana baada ya kusaini mikataba hiyo mipya mitatu kwa niaba ya Serikali na Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess kwa niaba ya Ujerumani, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, alisema fedha hizo zitaisaidia kukabiliana na athari za Uviko-19, kuboresha uhifadhi wa mazingira na huduma za jamii.
Alisema kuwa mkataba wa kwanza uliosainiwa unahusisha mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na mradi wa kuboresha huduma za afya uliiotengewa kiasi cha Euro milioni 16.5 sawa sh. bilioni 43.73.
“Katika fedha hizo kiasi cha Euro milioni sita kitatumika kuboresha huduma ya maji kwenye miji ya Mbeya, Songwe na Tunduma ambapo zaidi ya watu 500,000 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo pamoja na kutoa ajira ya watu 2,000 katika sekta ya maji kwenye maeneo hayo,” alisema.
Alifafanua kuwa mradi wa uboreshaji wa huduma ya afya umetengewa Euro milioni 10.5 na una lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika mikoa ya Tanga na Mbeya.
Tutuba alisema mradi mwingine unaofadhiliwa na Ujerumani una thamani ya Euro milioni 8.5 sawa na sh. bilioni 22.53 zitakazotumika kufunga mitambo maalumu ya kidigitali itakayosaidia kudhibiti magari ya watalii yanayoingia kwenye Hifadhi za Taifa yasiharibu mazingira katika Hifadhi nne za Serengeti, Burigi-Chato, Katavi na Mikumi.
“Mkataba wa tatu tuliosaini unahusisha msaada wa Euro milioni 20 sawa na sh. bilioni 53 zilizotolewa kama fedha za dharura kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa fedha uliotokana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19, katika sekta ya maliasili na utalii,” alieleza.
Alisema kusudi la mradi huo ni kufidia mapato yaliyopotea kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Misitu Tanzania (TAWA), katika maeneo tengefu katika Pori la Akiba la Selous na Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.
Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani, Regine Hess, alisema nchi yake inajivunia uhusiano wa kindugu uliopo kati ya nchi yake na Tanzania ulifikisha miaka 60 sasa na kwamba nchi hiyo itaendelea kutoa misaada zaidi kwa nchi.
Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani uliofanikisha upatikanaji wa msaada, Marcus Von Essen, alisema Ujerumani imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Na BENNY MWAIPAJA, Dar es Salaam