SERIKALI imesema itaendelea kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina bila kuchoka, kwa kuwa ofisi hiyo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Pia, imeipongeza ofisi hiyo kwa kazi nzuri ya usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma, maeneo ambayo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kuleta tija na kuendelea kutoa mchango wa ukuaji uchumi na kustawisha maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa Mwaka 2021/2022, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukaribishwa na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto, Dk. Ndumbaro alisema; “Ni ukweli usiopingika kutokana na majukumu makubwa ya kusimamia takribani Mashirika na Taasisi za Umma 237, Kampuni 50 ambako serikali imewekeza mtaji wake kwa utaratibu wa Hisa.
Pamoja na kusimamia jumla ya Mashirika ya Umma, viwanda na mashamba 341 yaliyobinafsishwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.”
Alisema watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wanapaswa kuzingatia kuwa nchi inawategemea katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kupunguza matumizi na kuimarisha utawala bora kupitia usimamizi madhubuti wa Mashirika na Taasisi za Umma.
“Kila mtumishi katika Ofisi ya Msajili wa Hazina anapaswa kutambua wajibu wake kwa taifa na kujitambua ana umuhimu katika kuwezesha taifa kufikia malengo yake.
“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, weledi na uzalendo mkubwa katika kusimamia rasilimali za umma mlizopewa dhamana ya kuzitunza na kusimamia ili zilete tija na kuongeza mapato yasiyo ya kodi kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kuwa na uwezo wa kuboresha huduma kwa wananchi na maslahi ya Watumishi wote,” alisema.
Awali,Mgonya alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuwa Msajili wa Hazina ili kuendeleza jukumu la usimamizi wa rasilimali za nchi zinazotokana na uwekezaji wa serikali.
Katika mkutano huo, Msajili wa Hazina aliwasilisha mambo mbalimbali ambayo ofisi imeyatekeleza katika kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma.
Pia aliwasilisha mikakati iliyopo katika kuimarisha usimamizi kwenye Mashirika na Taasisi za Umma ili mchango wa uwekezaji wa serikali ulete tija kwa maendeleo ya nchi.
Alisema ufanisi wa usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina umejidhihirisha katika maeneo mengi, akitolea mfano ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kuwa, katika kipindi cha miaka minne cha kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21 mapato yameongezeka kutoka Tsh. bilioni 161.03 mwaka 2016/17 hadi Tsh. bilioni 637.67 mwaka 2020/21.
Na Mwandishi Wetu