TANZANIA inaongoza kuwa na gharama za chini zaidi za huduma ya mtandao katika eneo zima la Afrika Mashariki na kati.
Wastani wa gharama za data nchini ni takribani senti 75 za kimarekani kwa Gigabaiti moja ya data ambapo kwa mujibu wa taasisi ya Cable.co.uk ya Nchini Uingereza, ndio bei rahisi zaidi katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari, hivi karibuni alisema tafiti nyingi za Kimataifa zimebainisha kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye gharama nafuu zaidi za Mawasiliano ya Simu na data barani Afika na Ulimwenguni.
Alisema Tanzania inashika nafasi ya 32 duniani miongoni mwa nchi za gharama za chini zaidi za data kwa ajili ya Intaneti.
Pia, upatikanaji wa gharama nafuu za data kwenye simu ni miongoni mwa mafanikio hayo; ambapo tafiti kadhaa zimebainisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye gharama nafuu na ya chini ya data.
“Bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola za Kimarekani (USD) 0.750 sawa na sh.za Kitanzania 1,725,”alifafanua.
Dk. Bakari alisema Barani Afrika Tanzania imo miongoni mwa nchi sita kinara kwa unafuu wa gharama ya data inayotumika kwenye simu, hatua hii ni muhimu ikizingatiwa serikali imekuwa ikiweka mazingira wezeshi ya uwepo watoa huduma wengi wa mawasiliano ya simu.
Pia uwingi wa makampuni ya utoaji huduma za simu umeleta ushindani ambao sasa unawezesha kushusha bei za mawasiliano ya simu pamoja na data.
“Kati ya mwaka 2015 na Februari mwaka 2022 bei ya mawasiliano ya simu zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 88 kwa mujibu wa Mamlaka ya udhibiti wa Mawasiliano nchini,” alieleza.
Alisema Tanzania inashika nafasi ya sita kwa unafuu zaidi wa gharama ya data kati ya nchi 52 barani Afrika.
Alifafanua kuwa katika eneo la Afrika Mashariki, Tanzania imeziacha mbali nchi jirani za Kongo, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Malawi, Zambia pamoja na Msumbiji.
Hata hivyo Alisema tafiti za Kimataifa zimebainisha nchi za Kongo na Kenya ndio zenye gharama kubwa zaidi kwa Afrika Mashariki, huku Malawi ikiwa na gharama kubwa kupita nchi zote za kusini mwa Afrika.
Na MWANDISHI WETU