POLISI Mkoa wa Pwani, imewakamata watu 4,450 kwa tuhuma za kutenda makosa ya barabarani.
Imeelezwa watuhumiwa hao walikamatwa kuanzia Julai 31 hadi Agosti 9, mwaka huu, mkoani humo na kutozwa faini za papo kwa papo zenye thamani ya sh. milioni 133.
Akizungumza mjini Kibaha na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani, Kamishna Msaidizi, Wankyo Nyigesa, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni iliyofanyika kipindi hicho.
Wankyo alisema magari mabovu 1,020 yalikamatwa na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria na zilikamatwa pikipiki 389 zenye makosa mbalimbali.
Mbali na hilo, kamanda huyo alieleza kuwa jeshi hilo limeokoa mali zilizoibwa baada ya mtuhumiwa kuvunja nyumba usiku, huku makosa mengine ya jinai yakiripotiwa vituoni.
Wakati huo huo, kamanda huyo alisema watuhumiwa 50 walikamatwa kwa makosa mbalimbali, ambapo kati ya hao, wanane walikuwa wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Bangladesh.
Aliyataja makosa mengine yaliyokuwa yakiwakabili watuhumiwa hao ni kukutwa na bangi puli sita, misokoto 12 na kete 315, bonanza tatu, redio mbili aina ya Sea Peano na spika tano mbili aina ya LG, lita 380 za mafuta ya transfoma, gongo lita 15 na runinga mbili.
Wankyo alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kutii sheria bila shuruti na kutoa taarifa za uhalifu wa aina yoyote ili wahusika wachukuliwe haraka hatua.
Na Scolastica Msewa, Kibaha