POLISI Mkoa wa Geita inamshikilia mwanaume mwenye umri wa miaka (30) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake, Ester John (28), mkazi wa Ibamba, wilayani Bukombe na mtoto wake, akidai kuwa binti huyo akuwa muaminifu.
Akizungumza kwa njia ya simu na UhuruOnline, Kamanda wa Polisi, Mkoani Geita, Henry Mwaibambe, amesema wanamshikilia mtuhumiwa huyo (jina linahifadhiwa) kwa mauaji ya mpenzi wake.
Amebainisha kuwa, mwanamke huyo ambaye kwa sasa ni marehemu aliondoka nyumbani kwake Juni 13, mwaka huu, akiwa ameambatana na mtu anayesemekana ni mpenzi wake.
Ameeleza kuwa, mwanaume huyo alimteka nyara binti huyo kisha kumuua na baada ya kufanya mauaji hayo aliwapigia simu wazazi wa marehemu akihitaji kulipwa fedha alizokuwa akimuhudumia kwa ahadi ya kumuoa huku akidai kuwa marehemu hakuwa muaminifu.
“Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kumteka nyara mwanamke huyo akishinikiza kulipwa gharama alizotumia kumtunza kwa ahadi ya kuoana baada ya kubaini siyo mwaminifu, aliposhindwa kumrudishia fedha yake ndipo alichukua uamuzi wa kumuua na kumzika katika Kijiji Masota, Wilaya ya Bukombe,” amesema Kamanda Mwaibambe.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwambaimbe, amesema mtuhumiwa aliwaongoza askari hadi eneo alikomzika Ester ambapo hatua za kisheria zilifuatwa kwa kufukua kaburi na kufanya uchunguzi wa utambuzi wa mwili wa marehemu.
Amesema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na ukikamilia mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
“Jina la mtuhumiwa tunalihifadhi kwa sababu ya upelelezi na hapa naelekea porini kufuatilia mwili wa mtoto wa marehemu ambaye mtuhumiwa amekiri kumuua baada ya kumuua mama yake” amesema.
Na BALTAZAR MASHAKA, Geita