POLISI Kanda Maalumu ya Tarime-Rorya, inamshikilia mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Tarafa ya Ingwe, Tarime mkoani Mara, Samwel Samwel, kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili akiwemo mkwewe wakiwa baa.
Inadaiwa mtuhumiwa aliwaua watu hao kwa kuwapiga risasi usiku wa kuamkia Jumapili, alipokuwa akiamulia ugomvi.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, ACP William Mkonda, amethibitisha Mei 23, 2022, kuhusiana na tukio hilo na kuwataja waliofariki dunia ni kijana aliyemuoa binti wa mtuhumiwa, Mwita Sibora na Chacha Bukima.
“Ni kweli watu wawili, wakazi wa Nyamongo, tarafa ya Ingwe, wilayani hapa, Mwita Sibora na Chacha Bukima wameuawa kwa kupigwa risasi na Samwel Samwel usiku wa kuamkia Mei 22, mwaka huu, wakati wakinywa pombe katika baa ya Charles Machage iliyoko kijiji cha Kewanja,” alisema.
Aliongeza: “Samwel aliyekuwa na bastola aliingilia kati ugomvi huo wa Mwita Sibora na Chacha Bukima kwa kufyatua risasi hewani na zingine kuwapata Sibora na Bukima waliokuwa wakigombana na kusababisha vifo vyao papo hapo.”
Mkonda alisema baada ya tukio hilo, walimkamata mtuhumiwa na wanaendelea kumhoji na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Alisema miili ya marehemu ilipelekwa Kituo cha Afya Sirari kwa uchunguzi na baada ya hapo itachukuliwa na ndugu zao kwa mazishi.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wamiliki wa baa kuwakagua wateja iwapo wana silaha ili wawatunzie hadi wanapotaka kuondoka kwa kuwa matukio mengi ya watu wenye silaha za moto hutokea katika ulevi na kusababisha madhara.
Aidha, aliwataka wanaomiliki silaha kufuata sheria na kuacha kuzitumia ovyo kwa kuumiza wenzao ambao ni tegemeo kwa familia zao na taifa.
Na Samson Chacha, Tarime