MKAZI wa Mpanda Hotel, Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wille Mwakapimba, amekutwa amefariki dunia, kwa kujinyonga chumbani kwa mpenzi wake, Hawa Ayubu.
Imeelezwa kuwa Mwakapimba, ameacha ujumbe usemao; amesikia sauti ya mama yake ambaye ni marehemu ikimtaka aende kufukua vitu vya kishirikina vilivyofukiwa katika kaburi lake.
Polisi mkoani humo, juzi ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi zaidi unaendelea.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivukoni, Kata ya Shanwe, Michael Sikenyenzi, alisema lilitokea saa 4.15 asubuhi, ikiwa ni muda mfupi tangu Mwakapimba kurejea kutoka Kituo cha Polisi, Wilaya ya Mpanda.
Sikenyezi alisema alipata taarifa za tukio hilo, baada ya kupigiwa simu iliyomtaka aende nyumbani kwa Hawa, ambako kuna mtu amejinyonga.
“Baada ya kufika nyumbani kwa Hawa nilikuta mwili wa marehemu ukining’inia chumbani, hivyo nililazimika kutoa taarifa polisi,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Baada ya polisi kufika eneo la tukio waliingia chumbani ambako walikuta ujumbe wa maandishi aliokuwa ameandika marehemu uliokuwa ukieleza alisikia sauti ya marehemu mama yake ikimtaka aende katika kaburi lake akafukuwe kwa kuwa kuna vitu vimefukiwa na ndugu yake ambaye amekuwa akiwafanyia ushirikina.”
Alisema baada ya kusoma barua hiyo, polisi waliwahoji ndugu wa marehemu waliokuwa wamefika eneo la tukio akiwemo kaka yake mkubwa.
Mwenyekiti huyo alidai kaka huyo alieleza kwamba marehemu alikwenda makaburi ya Mwangaza kufukua na kukuta kichwa kinachosadikiwa cha binadamu, sehemu ya siri ya mwanamke, sanda na kitambaa chekundu ambavyo alivichukuwa na kuvipeleka dukani kwa ndugu yake aliyekuwa akimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Alisema baada ya kuvipeleka vitu hivyo katika duka hilo lililoko Mtaa wa Mpanda Hoteli, Polisi walipata taarifa ya tukio hilo, ambapo walimkamata Mwakapimba kumweka mahabusu.
Aliyekuwa mpenzi wa Mwakipamba, Hawa alisema walikuwa wakiishi kama mume na mke katika nyumba aliyoachiwa na marehemu mume wake.
Hawa alieleza kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na Mwakapimba akimwomba arejee nyumbani haraka, lakini alipofika alimkuta amejinyonga.
Na IRENE TEM, Katavi