Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, wakati akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasimali Watu katika utumishi wa umma.
Ummy amesema katika nafasi hizo, waombaji walikuwa wengi na mchakato ulifanywa kwa haki, hivyo waliopita watatangazwa wakati wowote.
“Katika mchakato wa kupitisha majina, ofisi yangu ilisimamia kazi hiyo na waombaji walitendewa haki, hatukuangalia ‘vimemo’ kutoka kwa wakubwa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewaelekeza viongozi kuweka utaratibu wa kuwasikikiza watumishi wa chini ili kuongeza tija.
Pia, amewataka kuzingatia sheria inayoongoza Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuzipa umuhimu sekretarieti za mikoa kwa kuweka watu wenye uwezo ambao watafanyakazi bila uwoga na kwamba wanahitajika watu wenye uzoefu na weledi.
Ummy amefafanua kuwa serikali inatarajia kuanza kutoa posho ya mafuta kwa ajili wa watendaji na maofisa tarafa ili kuwapunguzia mzigo.
“Serikali itabeba mizigo wa kulipa posho za madiwani katika halmashauri 168 nchini, udhibiti wa mapato ya serikali unaendelea ili kuboreshà maeneo yenye uhitaji,” amesema Ummy.
Amewataka viongozi wanapokutana katika vikao mbalimbali kuhimiza watumishi kudai risiti za malipo pindi wanaponunua bidhaa ili fedha hizo zitumike katika shughuli na miradi ya maendeleo nchini.
“Ili tuweze kufanikiwa katika utendaji kazi wetu, lazima tuwe na motisha kwa watumishi wa chini tunaowahudumia, tunajisahau sana, tunakuwa wabinafsi wa kujiangalia sisi bila kuwajali watu wa chini yetu,” amesema.
Ummy amesema kiongozi anatakiwa kuongoza njia na kujenga utamaduni wa kusikiliza watu anaowasimamia kulingana na mapungufu yao, huku kiongozi bora akimtaja kuwa ni anayewaelewa vyema anaowaongoza na kuwasimamia na sio kuwahukumu.
Awali, Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laulean Ndumbaro amewataka watendaji hao kubuni mikakati ya namna ya kutoa motisha kwa watumishi.
Dk. Ndumbaro amesema wanaweza kutoa motisha kwa kutumia mbinu za kutengeneza vyeti, kuandika barua zenye lengo la kutambua watu wanaofanyakazi kwa bidii, kujituma na kujitoa katika taasisi zao huku wakibuni mbinu za kuwarekebisha watumishi wazembe.
Na HAPPINESS MTWEVE