MKAZI wa Kijiji cha Ihombe, Halmashauri ya Wilaya Mbeya, Mashaka Saimon (35), amejiua kwa kujichoma moto nyumbani kwake.
Saimon hivi karibuni aliokolewa na majirani wakati alipofanya jaribio la kujichoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli akidai kuchoshwa na maisha baada ya kutelekezwa na mke wake.
Akizungumzia tukio hilo mkoani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa Mbeya, Ulrich Matei, alisema tukio hilo limetokea Novemba 8, mwaka huu, saa 3:00 asubuhi, katika kijiji hicho kilichopo Kata ya Utengule Usongwe.
Matei alisema mwili wa Saimon ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Yokonia, ulikutwa ndani ya nyumba yake ukiwa umeungua moto.
“Marehemu alikuwa akisumbuliwa na maradhi muda mrefu na alitelekezwa na mke wake, hali iliyopelekea kukata tamaa ya maisha,” alisema Matei.
Kamanda huyo wa polisi alisema siku chache zilizopita, Saimon alifanya jaribio la kujilipua kwa kutumia mafuta ya petroli, lakini aliokolewa na mdogo wake.
Matei alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu au watu wenye hali ya kukata tamaa ya maisha kwa viongozi wao wa vijiji na mitaa kabla ya kutokea madhara kama iliyotokea kwa Saimon.
Na SOLOMON MWANSELE, Mbeya