POLISI Mkoa wa Katavi, inashikilia mkazi wa mtaa wa Maridadi, Kata ya Majengo, Manispaa ya Mpanda, Mashaka Sokoni kwa tuhuma za wizi wa misalaba 35 ya vyuma katika makaburi kwa lengo la kuuza kama vyuma chakavu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga mtuhumiwa huyo, alikamatwa Agosti 07, mwaka huu saa tano usiku.
“Siku ya tukio, mtuhumiwa alikutwa akiwa na kifurushi amebeba mgongoni, askari wa kikosi kazi maalumu cha polisi walipomuona walimtilia shaka,” alieleza.
Aliongeza kuwa: “Alipofanyiwa upekuzi kubaini kilichopo ndani ya kifurushi hicho, mtuhumiwa alikutwa akiwa na vipande 35 vya vyuma vya misalaba ambavyo alishafuta majina ya marehemu.”
Kamanda Kuzaga alieleza kuwa, baada mtuhumiwa huyo kuhojiwa, alikiri kuiba vyuma hivyo vya misalaba katika makaburi yaliyopo Nsemlwa, Manispaa ya Mpanda.
“Lengo la mtuhumiwa kwenda kuiba kwa kung’oa misalaba katika makaburi ni kutaka kujipatia kipato cha fedha kwa kuuza kama vyuma chakavu,” alisema.
Alisema msako mkali unaendelea kufanyika kwa kuwakamata washiriki wote wenye tabia ya kujipatia kipato isivyo halali kwa kufanya vitendo vya aibu kama hicho katika jamii.
Alisema mtuhumiwa bado anaendelea kushikiliwa na polisi akihojiwa zaidi na uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Na George Mwigulu, Katavi