MCHUNGAJI wa Kanisa la Zumaridi, Diana Bundala (39) maarufu kama ‘Mungu’ Zumaridi Mfalme, anashikiliwa na polisi mjini Mwanza, kwa kosa la usafirishaji haramu wa binadamu na unyonyaji.
‘Mungu’ Zumaridi, alikamatwa Februari 26, mwaka huu, saa 6:30 mchana, katika Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa, wilayani Nyamagana, jijini hapa.
Inadaiwa Mchungaji huyo alikutwa akiwatumikisha watu 149 aliowafungia ndani.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kusema kuwa kati ya watu anaodaiwa kuwatumikisha 57 ni wanaume 57 na 92 wanawake wakiwemo watoto 24 wenye umri kati ya miaka 4 hadi 17.
Ng’anzi alisema wanaodaiwa kutumikishwa aliwasafirishwa kutoka sehemu mbalimbali, kisha kuwafungia nyumbani kwake, ambako alikutwa akiwatumikisha kinyonyaji.
“Watu hao 149 wakiwemo watoto 24 wenye umri wa kati ya miaka minne hadi 17, wamekatishwa masomo kinyume cha sheria na amekuwa akiwaaminisha kuwa yeye ni ‘Mungu’ anayeponya, kufufua wafu na kutatua matatizo yao,” alisema.
Alifafanua kuwa kukamatwa kwa Zumaridi kunatokana na amri ya Mahakama ya Mwanzo Mkuyuni, iliyoamuru kumkamata mama mzazi wa mtoto Samir Ally aliyetakiwa kufikishwa mbele ya mahakama hiyo akikabiliwa na kesi ya kumfanya mtoto wake asiende shule.
Katika utekelezaji amri hiyo, polisi walifika nyumbani kwa Zumaridi anakodaiwa kuwepo kwa mzazi wa mtoto huyo aliyetakiwa kufikishwa mahakamani.
“Baada ya askari kufika eneo la tukio, mtuhumiwa Zumaridi akiongoza wafuasi wake waliwashambulia na kuwazuia kufanya kazi yao ya kumkamata mama huyo. Askari ilibidi waondoke eneo hilo kwa nia ya kutotumia nguvu ambayo ingeleta madhara,” alisema.
Kamanda huyo alisema Februari 26, mwaka huu, saa 6:30 mchana, polisi walirudi nyumbani kwa Zumaridi na kufanikisha ukamataji kwa mujibu wa sheria na kuwaokoa waliokuwa wamefungiwa wakitumikishwa kinyonyaji.
Ng’anzi alisema kanisa la Zumaridi lililoko Kata ya Butimba lilishafungiwa, hivyo upelelezi wa kina unaendelea ili kubaini kiini cha watu 149 wakiwemo watoto kukusanyika katika nyumba ambayo siyo ya ibada wala sehemu rasmi ya mkusanyiko wa kidini au kongamano
“Baada ya upelelezi mtuhumiwa na washirika wake watafikishwa mahakamani kwa tuhuma zikiwemo kuwashambulia na kuwazuia askari kufanya kazi waliyotakiwa kutekeleza kwa amri ya mahakama ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema.
Alionya na kutoa wito kwa baadhi ya watu kuacha kutumia mwamvuli wa dini kuhadaa watu kuwa wanapokuwa na matatizo ya kijamii hususan magonjwa, hali ngumu ya maisha, wanaweza kuwatatulia huku wakiwatumikisha, jambo ambalo ni upotoshaji na unyonyaji.
Katika hatua nyingine, Polisi mkoani Mwanza imewaachia kwa masharti watuhumiwa 36 wa makosa ya vitendo vya kujihusisha na ugaidi, baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
Kamanda Ng’anzi alisema kuachiwa kwa watuhumiwa hao ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ya kuwachia watuhumiwa hao kwa masharti.
Alisema pamoja na dhamana, kila mtuhumiwa atatakiwa kuripoti Polisi Mkoa mara mbili kwa mwezi.
Na PETER KATULANDA, Mwanza.