MKAZI wa Kijiji cha Ilunga, Kata ya Iyenze wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Limi Kulwa (30) ,ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake akituhumiwa kujihusisha na ushirikina.
Kamanda wa Polisi wa Shinyanga, George Kyando, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mauaji hayo yalitokea Septemba 27, mwaka huu , saa 2.30 usiku.
“Kulwa alikatwa na panga kichwani, usoni, mikononi na mtu ambaye tunaendelea kumtafuta baada ya kutekeleza mauaji hayo na kutoroka,”alisema.
Alisema chanzo cha mauaji hayo kimetokana na imani za ushirikina, ambapo mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu marehemu kwa kumroga na kumuua baba yake Kulwa Lusana (60) ambaye alifariki dunia Julai, mwaka huu.
“Mtuhumiwa alimvizia Kulwa wakati anapika chakula nyumbani kwake na kumshambulia kwa panga na kisha kutokomea kusikojulikana,” alisema Kyando.
Alifafanua kuwa katika eneo la tukio, limeokotwa panga moja lenye damu .
Kyando amewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
“Mauaji Shinyanga hayana nafasi tena, tutawakamata wote waliotekeleza mauaji haya na tutawafikisha mahakamani, wananchi achaneni na imani hizi za ushirikina,”alisema.
Na SALVATORY NTANDU, KAHAMA