POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inamshikilia Haji Mussa (30) kwa kumshambulia kwa fimbo na kumsababishia maumivu makali mtoto wake wa kambo aitwaye Feisali Masawe (11), kwa madai ya kuiba sh.195,000.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema kuwa, mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Chamazi Temeke, Dar es Salaam ambapo mnamo Februari 22, mwaka huu usiku, anatuhumiwa kufanya tukio hilo.
Kamanda Muliro alisema Februari 23, mwaka huu, mwanafunzi huyo alifika shule, ilipofika saa 6.30 mchana, alianguka na kupoteza fahamu.
“Feisali ni mwanafunzi wa darasa la tatu, Shule ya Msingi Chamazi Dovya, ameshambuliwa na baba yake wa kambo kwa madai ya kuiba sh. 195,000 kisha kusababishiwa maumivu makali maeneo mbalimbali ya mwili wake,” alisema.
Muliro alisema kwamba, baada ya kupoteza fahamu, alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu .
Alisema kwamba, uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha mtoto huyo kuumwa ni kipigo alichokipata kutoka kwa Baba yake wa kambo.
“Kitendo alichofanya mtuhumiwa ni cha kikatili, Jeshi haliwezi kuvumilia vitendo hivyo, kwa sababu hiyo, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Polisi Kanda hiyo linawashikilia watuhumiwa 12 kwa madai ya kujihusisha na uhalifu mtandaoni.
“Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mikoa mingine na mamlaka za Serikali, limefanya msako maalumu kuanzia Februari 06 hadi 20, 2022 na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12 akiwemo Rajabu Hamisi (34), Mnyaturu, mkazi wa Rau Moshi Kilimanjaro na wengine 11 ambao wamekuwa wakijihusisha na makosa ya wizi mtandaoni,” alisema.
Watuhumiwa hao walikutwa na Laptop moja mali ya Kampuni ya Tigo, EFD mashine moja, Simu za mkononi 42, kadi za Tigo 55, nyaraka zenye kurasa 1,500 ambazo ni taarifa za Mawakala wa mtandao wa Tigo nchi nzima na nyaraka zenye taarifa za wateja wa CRDB.
Kamanda Muliro alisema vielelezo vyote hivyo, walikuwa wakivitumia kufanyia wizi kupitia kwa mawakala na mteja mmoja mmoja kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wakijifanya ni wafanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi.
Pia, walikuwa wakitoa maelekezo ambayo husababisha mteja au wakala kuwatumia fedha wahalifu hao na wakati mwingine, wahalifu hao, hutoa maelekezo kwa kujifanya wanahuisha mfumo wa kampuni wanaokutajia.
“Mwishowe huelekeza kuweka namba yako ya siri baada ya hapo mhusika hujikuta ameibiwa fedha kutoka katika akaunti yake,” alisema.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawataka watu wote walioibiwa kwa njia ya mfumo huo, wafike Kituo cha Polisi Oysterbay ambako upelelezi wa watu hao unaendelea ili utaratibu wa kisheria ukamilishwe na watuhumiwa wafikishwe mahakamani.
Na ATHNATH MKIRAMWENI