MKUU wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani, amewaagiza wasimamizi wa miradi ya ujenzi miundombinu inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 kuwa makini na matumizi ya fedha hizo ili zitekeleze malengo yaliyokusudiwa.
Alisema ni vyema kila hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo wakaweka utaratibu wa kuchukua picha ya hali halisi ili kudhibiti udanganyifu unaoweza kufanywa na baadhi wasimamizi wasiokuwa waaminifu.
Balozi Dk. Batilda alitoa kauli hiyo, wakati kikao cha kawaida cha robo ya kwanza ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo.
Alisema picha zisipochukuliwa kabla ya ujenzi kuanza, baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wanaweza kukarabati maboma ya zamani na kudai wamejenga majengo mapya.
Balozi Dk. Batilda, alisema kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu inayotokana na fedha zilizotolewa na serikali inaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, lazima ziwe wazi na miradi yote ipigwe picha.
“Tushirikiane kusimamia ujenzi wa miundombinu ili iwe na ubora kama alioulenga Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha anaboresha sekta ya elimu na afya, fedha mzione kama kaa la moto ni lazima zifanye kazi iliyokusudiwa,” alisema.
Alisema ili kufanikiwa hilo, kila halmashauri lazima iunde kamati ya uratibu na ufutiliaji na kila baada ya siku nne itote taarifa kwa katibu tawala wa mkoa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa miradi yao.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora, aliwaagiza wakurugenzi kuhakikisha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule za sekondari na shule shikizi inakamilika.
Balozi Dk. Batilda alisema lengo la serikali ni kuhakikisha watoto watakuwa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza hapo mwakani wanaanza masomo kwa pamoja ili kuondokana na kuanza kwa awamu.
Na Mwandishi Wetu