JENIPHER LUKONGE NA SITI KHALIFA (PSJ)
MKAZI wa Mburahati, jijini Dar es Salaam, Ombeni Zacharia amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu shitaka la kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi gramu 19.07.
Zacharia (18) alifikishwa mahakamani hapo juzi na kusomewa shitaka na Wakili wa Serikali, Debora Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya.
Debora alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 15, mwaka huu, eneo la Mburahati, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alimweleza mshitakiwa kuwa shauri linalomkabili linadhaminika kwa mujibu wa sheria, hivyo anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaotia saini bondi ya sh. 500,000 kwa kila mmoja.
Mshitakiwa alifanikiwa kutimiza masharti hayo, hivyo aliachiwa kwa dhamana hadi Aprili 28, mwaka huu, kesi itakapopelekwa kwa usikilizwaji wa awali.