NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amewataka Watanzania kuondoa hofu kufuatia bei ya mahindi kupanda kwamba hakuwezi kusababisha upungufu wa chakula nchini kutokana na maandalizi makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Bashe ametoa kauli hiyo jijini Dodoma alipofanya ziara ya ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha ITRACOM Pertilizers Ltd kinachojengwa na mwekezaji kutoka Burundi nje kidogo ya Jiji ujenzi ambao umefikia asilimia 57.
Pia, Naibu waziri huyo amesema Serikali imejipanga vyema hivyo Taifa haliwezi kuingia katika njaa kwani wameweka maandalizi makubwa na kipo chakula cha kutosha katika hifadhi zilizopo nchini.
Bashe amesema hadi sasa kuna zaidi ya tani 200,000 ambazo hazijaguswa huku akisema akiba kwa wakulima bado iko ya kutosha huku akieleza kuwa kuna kitengo cha ufuatiliaji wa chakula kinaendelea kuratibu mwenendo wa chakula nchini.
“Licha ya uwepo wa uhaba wa mvua uliotangazwa na Mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa, iwe itakavyokuwa lakini chakula kilichopo kinaweza kuwatosheleza wananchi wenye uhitaji kwa akipindi kirefu.” amesema
Pia, amesema wanatarajia kufunga mipaka ya nchi kwa faida ya wakulima kwani kilimo ni biashara hivyo lazima wanufaike na matunda yao.
Kuhusu kiwanda hicho amewataka wabuni kwa kutumia teknolojia rafiki kwa udongo wa Tanzania ili wakulima waweze kunufaika badala ya kujutia mbolea watakayonunua kiwandani hapo.
“Nawaagiza wataalamu wa kilimo kukaa na wataalamu wa mwekezaji huyo mapema kabla ya kuanza kwa uzalishaji mwezi Julai ili wazungumze namna bora watakavyofanya kubaini maihitaji kwa kila eneo ili kiwango cha utengenezaji kilenge moja kwa moja mahitaji ya eneo husika.”amesema
Mhandisi Musafiri Dieudonne ambaye ni msimamizi wa mradi huo amesema wako kwenye hatua nzuri za kuelekea kuanza uzalishaji ambapo wameshashusha mashine zinazotakiwa kiwandani hapo kwa asilimia 75 akisema kasi yao inakwenda vizuri kutokana na ushirikiano wanaopata kutoka Serikalini.
Dieudonne ametaja changamoto ya kukatika kwa umeme kunakosababisha kushindwa kusukuma maji na vibali vya wafanyakazi kutoka Burundi kuwa ni sehemu ya vikwazo katika kufikia malengo waliyojiwekea.
Amesema uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya dola 180 milioni wakati kwenye uzalishaji wanalenga kuwa asilimia 60 ya kiwango cha mbolea itakuwa ni samadi na mpaka sasa kimeajiri watanzania 500 huku raia wa Kirundi wakiwa 100.
Oktoba 25,2021 Rais wa Burundi Everiste Ndaishimiye alitembelea kiwanda hicho na kuweka jiwe la msingi huku akisisitiza mashirikiano katika mradi huo unaotarajia kuzalisha tani laki 6 kwa mwaka na sehemu kubwa ya mbolea yake ni samadi.
Na Happiness Mtweve, Dodoma