WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, amewataka wakuu wa Mikoa Nchini kuwasilisha taarifa za ujenzi wa madarasa 15,000 yanayojulikana kama Madarasa ya Mama Samia kabla au ifikipo Januari 25, mwaka huu.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Mkutano wa Siku Mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
Bashungwa amesema ni lazima kila mkuu wa mkoa ahakikishe anawasilisha taarifa hizo kwa muda uliopangwa ili kuanza uchunguzi wa utekelezaji wa ujenzi wa madarasa hayo.
Amesema wakuu wa mikoa wanapaswa kujiridhisha kuhusu taarifa hizo kabla ya kuziwasilisha Tamisemi ili kubaini kama ujenzi wa madarasa hayo ulizingatia taratibu, miongozo na thamani ya fedha ilizingatiwa.
“Baada ya kazi nzuri ya ujenzi wa madarasa hayo 12,000 ya sekondari na 3,000 vituo shikizi kukamilika na wanafunzi kuanza masomo, kianchofuata ni kufanya uchunguzi kuhuau ujenzi wa madarasa hayo kama ulizingatia taratibu,” amesema.
Waziri huyo amebainisha kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi nzuri ya kuboresha elimu ya msingi hadi ngazi za juu kwa kutoa fedha kujenga madarasa 15,000, kitendo hicho kinaonesha nia nzuri ya Rais kuboresha elimu ya msingi na sekondari nchini.
Amesema Rais Samia ambaye ndiye waziri mwenye dhamana ya Tamisemi ametoa maagizo kwake kuhakikisha Tume ya Utumishi wa Walimu inaimarika ili kuongeza utendaji kusaidia walimu na kuondoa changamoto zinazowakabili watumishi hao ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya watumishi wote nchini.
Bashungwa ameipongeza Tume kwa kuchapa kazi nzuri kwani kati ya Julai 2020-Juni 2021 imepandisha madaraja walimu 126,346, pia imeajiri 14,949 na kutoa adhabu kwa walimu 1,795 waliokiuka maadili ya kazi.
Pia Bashungwa ameeleza kusikitishwa na kitendo cha walimu kukiuka maadili ambapo kati yao, 931 sawa na asilimia 51.9 wameadhibiwa sababu ya utoro, kitendo ambacho kinawanyima haki wanafunzi ya kusoma na kupata elimu bora.
Katika hatua nyingine ameagiza Tume hiyo kuendelea na kutoa adhabu kwa walimu wanaokiuka maadili hasa watoro ambao wanaacha vipindi na kuwafanya wanafunzi wakose masomo.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tume ya Utumishi ya Walimu, Profesa Willy Komba amempongezi Rais Samia kwa kujali sekta ya elimu nchini na kutekeleza Ilani ya CCM inayotaka serikali kuboresha elimu nchini hasa ya ufundi.
“Rais Samia amefanya mambo makubwa katika kipindi kifupi katika kuboresha elimu Tanzania pamoja na kujali elimu ya mtoto wa kike,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema TSC ambao ni wasimamizi wa walimu nchini watahakikisha ajira zinapatikana, nidhamu inadumishwa na walimu wanapata maendeleo ili kuwa bora na kulea wanafunzi vizuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama, amempongeza Rais Samia kwa kuwapandisha madaraja walimu wote waliokuwa na sifa ya kupanda katika kipindi cha Julai 2021-Juni 2022.
Na Happiness Mtweve, Dodoma