WAZIRI Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, amewashauri wananchi wa mkoa wa Kagera hasa viongozi kutoendekeza uongo, fitina, majungu, umbea na kusingiziana ambapo amewakumbusha kuwa, kazi ya siasa ni kusemeana mema, kupendana na kushikamana na kushughulikia kero za wananchi.
“Kazi ya siasa sio uongo na kuapizana eti kwakuwa wewe ni kiongzi utamshughulikia aliyepo chini yako bila hata sababu ya msingi kwasababu unauwezo wa kufika makao makuu, tuache tabia hizo tushirikiane kujenga nchi yetu” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa CCM mkoani Kagera ambayo yamefanyika leo Wilayani Karagwe.
Pia, ameshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za mapambano ya Uviko-19 ambapo Rais aliona awekeze katika masuala ambayo yatakuwa na faida kwa kizazi cha sasa na kijacho ambayo ni miundombinu ya Elimu na Afya.
Baadhi ya wanachama wa CCM mkoa wa Kagera wamemshukuru Rais Samia kwa kumpa nafasi ya Uwaziri wa TAMISEMI Waziri Bashungwa kwani hiyo ni Wizara kubwa na nyeti inayogusa maisha ya wananchi.
Wameahidi kumuunga mkono kwani kuaminiwa kwa Bashungwa inamaanisha mkoa wa Kagera ndio umeaminiwa huku wakimtaka waziri huyo kuchapakazi kwa uadilifu na uaminifu ili aendelee kujenga tabia ya kuaminika.
Na Angela Sebastian