ZAIDI ya Tsh. bilioni 10.8 zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini zikiwemo bilioni 8 za bajeti ya kawaida na bilioni 2 ambazo ni fedha za UVIKO-19.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, akiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Itilima iliyopo mkoani humo.
“Angalia kiasi cha fedha kilichowekwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwenye miradi ya maji katika miezi sita tumepokea zaidi ya bilioni 8 kwaajili ya miradi ya maji vijijini ndani ya mkoa huu ( Simiyu) na hii juzi ameongeza zaidi ya bilioni 2 za UVIKO-19 kwa ajili ya maji jumla kwenye maji peke yake tuna zaidi ya bilioni 10.8 ndani ya muda mfupi hakika serikali ya awamu ya sita imelishughulikia suala la maji kwa vitendo” amesema Kafulila.
Mbali na hilo amesema kuna mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa viztoria ambao maji yatafikishwa mkoani hapo kupitia bomba lenye urefu wa km 194 lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400 ambapo vijiji 244 vitanufaika.
“Hivi ni viashiria tosha vya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) ya kupeleka maji vijijini kufikia 85% kwenye vijiji kwa mkoa wa Simiyu tutavuka lengo kwa kufikia 90% uamuzi wa hekima na kimkakati wa Rais mawazo ya hekima kuzitumia fedha za UVIKO-19.
Fedha hizi zingeenda kwenye semina, kununua vitakasa mikono, barakoa yeye amezileta kwenye kununua magari ya kuchimba visima kila mkoa, mkoa wa Simiyu tunaenda kupata mitambo kupima maji yote haya ni maamuzi ya kimkakati” amesema Kafulila.
Kafulila amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka miwili upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 40.5 na sasa umefikia asilimia 67.5 sawa na ongezeko la asilimia 27.
Na Anita Balingilaki, Itilima