UJERUMANI imeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 71 (takribani sh. bilioni 190.5), kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, afya ya mama na mtoto na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Nyaraka za makubaliano ya msaada huo, zimetiwa saini jijini Dar es Salaam, Oktoba 26, 2021, kati ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayesimamia masuala ya Fedha za Nje, Amina Khamis Shaaban na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Ujerumani, Marcus Von Essen.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa nyaraka hizo, Naibu Katibu Mkuu, aliyataja maeneo yatakayonufaika na msaada huo ni afya ya mama na mtoto iliyotengewa Euro milioni 24 na mradi wa kuzuia migogoro kati ya wanyamapori na binadamu.
“Maeneo mengine yatakayonufaika na fedha hizi ni mpango wa kufidia upotevu wa makusanyo ya maduhuli katika sekta ya utalii kutokana na upungufu wa watalii walioingia nchini kwa sababu ya ugonjwa wa Uviko-19, kuzuia ujangili, kuboresha miundombinu katika makazi na jamii inayozunguka maeneo ya Hifadhi za Taifa, utakaogharimu Euro milioni 15,” alisema.
Alisema Euro milioni 20 zitaelekezwa kuboresha huduma ya maji katika miji inayokuwa na Euro milioni 3 zitatumika kuboresha usalama wa maji maeneo ya baadhi ya miji nchini.
Amina alisema kiasi kingine cha Euro milioni tatu, zitatumika katika masuala ya kulinda haki za akinamama na wasichana wanaokabiliwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa kuwapa msaada wa kisheria.
Aliishukuru Ujerumani kwa kuanzisha majadiliano na Tanzania baada ya kusitisha mijadala hiyo tangu mwaka 2015 na kuahidi kuwa, fedha zitakazotolewa, zitatumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.

Wakizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess na Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani ulioshiriki majadiliano yaliyofanikisha kupatikana kwa msaada huo, Marcus Von Essen, kwa nyakati tofauti walisema nchi hiyo, imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Walieleza chini ya makubaliano mapya, Ujerumani itajikita zaidi kusaidia afya ya mama na mtoto, kusaidia masuala ya bima ya afya kupitia NHIF, maji na usafi wa mazingira, usimamizi wa fedha za umma, kuhifadhi maeneo ya urithi wa dunia kama vile hifadhi ya Selous na kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya kikatili.
Aidha, walisema Ujerumani itarejesha mipango yake ya kusaidia miradi ya maendeleo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tayari nchi yao imeanza kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa maji visiwani humo.
Walisema kuwa nchi yao itatoa kiasi kingine cha fedha Alhamisi Wiki hii ambapo mikataba ya misaada kadhaa itatiwa saini kati ya nchi hiyo na Tanzania ikiwa ni mwanzo mpya wa kuhakikisha kuwa Ujerumani inashirikiana na Tanzania kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ninayo furaha Tanzania inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru, ni muda huo huo ambao Ujerumani na Tanzania zimekuwa katika ushirikiano ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Kiongozi wa Ujerumani wa wakati huo Profesa Grzymek,” alisema Balozi Regine Hess.
Alibainisha kuwa Ujerumani imeongeza ahadi zake kwa Tanzania kwa asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka uliopita na kwamba kutokana na hamu yake ya kutaka kuongeza zaidi misaada kwa Serikali ya Awamu ya Sita, imekuja na Msemo usemao “miradi zaidi, ufadhili zaidi”.
Kikao hicho cha majadiliano kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk. Juma Malik Akil ambaye aliishukuru Ujerumani kwa kufufua upya majadiliano kwa uamuzi wake wa kuanza kuisaidia Zanzibar katika kutekeleza miradi yake ya maendeleo.
Na BENNY MWAIPAJA