MKUU wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amesema upatikanaji wa maji mkoani humo utaenda kuongezeka kwa takribani lita milioni 1. 8 kwa siku ambapo mpaka sasa uzalishaji ni lita milioni 28 huku mahitaji yakiwa lita milioni 42.
Amayasema hayo baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba 24 uliofanywa kati ya RUWASA na wakandarasi, RUWASA na local fundi ambapo amesema ongezeko hilo litakwenda kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 6.4.
Aidha, amesema kwa mantiki hiyo upatikanaji wa maji mkoani humo utaongezeka kutoka asilimia 67.4 ya sasa hadi kufikia asilimia 73 miezi sita ijayo ambayo ni muda wa mkataba (miezi sita).
“katika malengo ya kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini kwasababu sisi ni mikoa ambayo zaidi ya asilimia 92 ni vijiji, tafsiri yake ni kwamba tutakuwa tumebakiza asilimia 12 tu ” amesema Kafulila na kuongeza kuwa :
” Ni vyema ikafahamika katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2021/22 bajeti ya maji kwa mkoa wetu (Simiyu) ni takribani bilioni 23.8 hiki ambacho tumekisaini leo ni bilioni 6.9 ni sehemu tu ya utekelezaji tafsiri yake ni kwamba kuna makubwa zaidi / kuna miradi mingine zaidi inakuja kusainiwa na yote hiyo itakuwa inatafsiri ongezeko la upatikanaji wa maji kwahiyo ni dhahiri kwamba serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan fedha kwaajili ya miradi maji sio mgogoro…. mgogoro hapa labda uwe jinsi ya kutekeleza / kusimamia” ameongeza Kafulila.
Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mhandisi Mariam Majala amesema katika mwaka huu wa fedha 2021/22 walikubaliwa kutekeleza miradi 52 ambayo ni 25 mipya ,15 ya ukamilishaji ,10 kwaajili ya upanuzi , miwili kwaajili ya ukarabati na kati ya miradi hiyo ( 52 ) 6 walikosa vyanzo na hivyo kwasasa wanatekeleza miradi 46 .
“Mkuu wa mkoa mbele yako leo utashuhudia utiaji saini wa mikataba 24 kati ya hiyo miradi 12 itasainiwa kati ya RUWASA na wakandarasi, miradi mingine 12 kati ya RUWASA malocal fundi katika wiliaya zote za mkoa wa Simiyu kwa jumla ya shilingi bilioni 6.9” amesema mhandisi Majala.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed amesema wao kama chama watapita kukagua utekelezaji mwezi wa tatu ambapo ameongeza kuwa wanachohitaji ni kukutana na kitu ambacho wamekisaini na sio kukuta vitu tofauti.
Dickson Mwipopo ni mkurugenzi wa Mponela Construction & Co LTD amesema ndani ya siku 14 atakuwa tayari kazini na kuahaidi kutekeleza kazi kwa wakati hata kabla ya miezi sita ya mkataba huku Mkurugenzi wa Jonta Investment LTD, John Ntalimbo akiishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuleta fedha za miradi ya maji ambayo imewasaidia kupata kazi na kuaidi kumaliza kazi kwa wakati ili kumtua mama ndoo kichwani .
Na Anita Balingilaki, Simiyu