BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 37,731 wa mwaka wa kwanza, waliopangiwa mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 99.9 kwa mwaka wa masomo 2021/2022.
Mwaka huo wa masomo, unatarajiwa kuanza rasmi wiki ijayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, akitangaza orodha hiyo, alisema kati ya wanafunzi hao, wanaume ni 23,379 sawa na asilimia 62 na wanawake 14,352 sawa na asilimia 38.
Badru aliongeza kuwa, HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wapate taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.
“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni…lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea, ili watimize ndoto zao,” alisema Badru.
ORODHA AWAMU YA PILI
Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya awamu ya pili, Badru alisema imepangwa kutolewa Oktoba 21, mwaka huu, baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.
“Orodha hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja…tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili Alhamisi, Oktoba 21, 2021,” alisema Badru.
SH.BILIONI 570 ZIMETENGWA
Kwa mujibu wa Badru, serikali imetenga sh. bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya jumla ya wanafunzi 160,000 ambapo kati yao, 70,000 watakuwa wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.
Wakati huohuo, Badru alisema HESLB imeshapokea fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na taratibu za malipo zimeanza ili fedha hizo ziwe zimefika vyuoni kuanzia kesho.
Aidha, alisema bodi hiyo inawasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.
Na MWANDISHI WETU