BODI ya Mikopo Tanzania (HESLB), imetangaza awamu ya nne yenye wanafunzi wapya 5,003 wa mwaka wa kwanza wa masomo watakaonufaika na mikopo hiyo ambapo zaidi ya sh bilioni 11.6 zitatumika.
Aidha, hatua hiyo imetajwa kuwa imetokana na mwaka huu wa masomo kuwa wa neema, kwani serikali imeongeza bajeti ya mikopo kutoka sh. bilioni 464 hadi sh.bilioni 570 kwa mwaka huu wa masomo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Badru, amesema orodha hiyo ya awamu ya nne ya wanufaika wa mikopo, inafikisha wanufaika kwa mwaka huu wa masomo kuwa 65,359 ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 168.9.
“Orodha hii ya nne ina wanufaika 5,003, ambao muda wowote kuanzia sasa wanaweza kuingiziwa pesa katika akaunti zao walizoombea mikopo na idadi ya wanufaika sasa ni 65,359 na kati yao yatima ni 1,133 ambao wamefiwa na wazazi wote wawili, huku wanafunzi 9,450 wakiwa wamefiwa na mzazi mmoja mmoja,”amesema.
Badru amesema kati ya wanafunzi hao 198 ni wenye ulemavu, 2,919 waliofadhiliwa na taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari na 51,559, wanaotoka katika kaya masikini zilizo chini ya Taasisi ya Kuhudumia Kaya Masikini (TASAF).
Amesema, kutokana na takwimu hizo ni wazi dhamira ya serikali kuwawezesha vijana kutoka kaya masikini imeonekana, kwakuwa mikopo hiyo imewagusa zaidi wasio na uwezo, ambapo kumekuwa na ongezeko kwa asilimia 41 ya wanufaika wote 65,359 ambapo wanawake ni asilimia 59.
Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, Badru amesema bodi inakamilisha malipo ya wanafunzi 74,440,ambao ni wanufaika wanaoendelea na masomo baada ya kupokea matokeo yao ya mitihani, yanayothibitisha kuwa wamefaulu kuendelea.
Alisisitiza kuwa, wanafunzi hao ni 98,000, ambao matokeo yao yamethibitishwa kuendelea hadi kufikia jana ni 74,440 na leo wataingiziwa fedha zao.
“Katika hatua nyingine tungependa kuwaeleza habari njema kuwa tunatarajia kuwa na awamu nyingine ya tano, hii ni pamoja na wale wanafunzi ambao walikata rufaa, hivyo dirisha la rufaa litafunguliwa Novemba 6 mwaka huu, ili kuwapa fursa wanafunzi hao,”alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi Elimu ya Juu (TAHARISO), Frank Nkinda, alisema wanaishukuru serikali kwa mikopo hiyo ambayo imetolewa kwa wakati na amewaasa wanafunzi kuwa wavumilivu.
Na Mariam Mziwanda