BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itawachukulia hatua watu wanaotumia vibaya noti katika shughuli za kijamii ikiwemo sherehe kwa kuzirusha sakafuni, kuweka katika mwili uliolowa jasho na kuzitumia kama mapambo.
Taarifa iliyotolewa na BoT kisha kusainiwa na Gavana wa benki kuu, Profesa Florens Luoga, ilieleza kuwa vitendo hivyo vinatweza fedha ya Tanzania ambayo ni moja ya tunu za taifa.
“Watu wamekuwa na tabia ya kutunza wahusika wa matukio kwa kuwarushia noti zinazoanguka sakafuni na muda mwingine kukanywaga, kuzivingilisha katika maumbo mbalimbali, kuitumia kama mapambo, kuweka katika mwili uliolowa jasho na matukio yote yanayofanana na hayo,” alibainisha.
Aliongoza kuwa: “Vitendo hivyo vinaendelea kutokea licha ya BoT na viongozi mbalimbali wa serikali kwa nyakati tofauti kuvikemea.”
Profesa Luoga alisema BoT inatoa onyo kwa wananchi ambao bado wanakaidi agizo hilo ambalo limetoka mara kadhaa, kuhusu namna sahihi ya kutunza noti za Tanzania zinazokuwa mikononi mwa wananchi kwa kuzitumia kinyume na maadili pamoja na matakwa ya kisheria.
“Kwa taarifa hii BoT itaanza kuchukua hatua dhidi ya wale wote watakaohusika na vitendo vya matumizi mabaya ya noti ya Tanzania kwa njia yoyote ile ikiwemo kuweka fedha sakafuni na sehemu yoyote ambayo sio nadhifu,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa gavana huyo alisema vitendo hivyo vinachangia kutweza fedha na kusababisha uchakavu hivyo kuongezea serikali gharama ya kuchapisha fedha zingine.
Alisema BoT inawashauri washiriki katika matukio yote ambayo yanahusisha matumizi ya fedha, kuandaa vyombo maalumu vya kuweka fedha hizo badala ya kufanya vitendo ambavyo havikubaliki.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa mara moja kwa benki kuu au vyombo vya usalama pale wanapobaini matumizi ambayo sio sahihi ya fedha ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
“Tukitunza fedha zetu tunachangia kuzifanya zitumike kwa muda mrefu, hivyo kuipunguzia serikali gharama za kuchapisha noti na kutengeneza sarafu mpya kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” alieleza.
Na MWANDISHI WETU