WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamesema wamebaini kuna changamoto katika utoaji huduma katika mifumo ya mtandao hali inayosababisha baaadhi ya wananchi wa pembezoni kutofikiwa ipasavyo.
Hatua hiyo imetajwa kuwa inatokana na kutokuwapo na elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya mifumo hiyo, hivyo ipo haja kupanua wigo ili kuwafikia watu wengi.
Akizungumza Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa, amesema pamoja na kutoa huduma za usajili katika mifumo ya mtandao wapo baadhi ya wananchi hawafikiwi na huduma.
Amesema ushiriki wa Wakala hao katika maonyesho, umekuwa na tija kwakuwa wamewafikia watu wengi zaidi ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu upatikanaji wa huduma katika mitandao.
“Katika maonyesho haya tumeweza kusajili kampuni, kutoa leseni za biashara,leseni za viwanda na huduma za ufumbuzi wa kihabari,” amesema.
Amebainisha kuwa, wapo baadhi ya watu waliofika katika maonyesho hayo walikuwa hawajui kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii katika kupata huduma, hivyo wale waliofika na vielelezo vinavyohitaji na kutimiza masharti wameweza kupatiwa vyeti vya usajili hapohapo.
Pia Andrew, amesema wamejifunza na kupokea changamoto nyingi ambazo wanaenda kuzifanyiwa kazi.
“Hatua za haraka tutakazochukua ni kujikita katika kutoa elimu, kwakuwa uhitaji ni mkubwa kuhusu umuhimu wa kusajili biashara na kampuni,”amesema
Ameongeza kuwa, katika hatua nyinyine wameanza kutoa elimu kwa maafisa biashara katika halmashauri, ili kukidhi mahitaji ya jamii katika kanda mbalimbali, lengo likiwa ni kutoa fursa kwa kila mwenye uhitaji kufikiwa.
Aidha, ameitaka jamii kutambua madhara ya kutokusajili biashara na kampuni ni pamoja na kukiuka sheria, kujinyima fursa ya kuwa rasmi na kutambulika kisheria, kwakuwa dunia inabadilika na watu wanatumia nafasi hiyo kujipatia mikopo.
Andrew, amesema wanayo mikakati mingi ya kufikia jamii ikiwemo kutoa huduma katika viwanja vya wazi maeneo tofauti.
Na REHEMA MAIGALA