WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), umewataka wananchi kuepuka kutapeliwa wakati wa usajili bali wawatumie watu sahihi ili kupata huduma wanazozihitaji.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Ofisa Leseni kutoka Brela, Saada Kilabula, wakati wa Maonesho yajulikanayo kama ‘Kamilika 2022’ yanayoendelea Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Amesema taasisi hiyo imekuwa ikikutana na watu mbalimbali ambao wanadai kutapeliwa na watu ambao sio wa Brela kwa maelezo kuwa wanawasaidia ili wapate huduma wanazohitaji.
Ofisa huyo ametaja changamoto nyingine ni wateja wao kutokujua utumiaji wa Teknolojia wakati wa usajili kwa kuwa sasa wakala huo unatumia mtandao katika kujisajili.
“Wananchi kutikujua matumizi ya mtandao ndio sababu inayotufanya tutoke ofisini tuje kuwafuata ili kutatua changamoto za kimtandao wanazokutana nazo,”amesema.
Pia tangu kuanza kwa maonesho hayo wamesajili jumla ya wananchi 1000 ambao walisajili majina ya biashara.
Mbali na majina ya Biashara walisajili kampuni, alama za biashara na huduma, leseni za viwanda, leseni za biashara kundi A na utoaji wa baraza ambapo mteja anapewa cheti mara tu baada ya kukamilisha usajili.
Pia Brela katika maonesho hayo inatoa huduma ya kuwasaidia wale wenye matatizo mbalimbali ya kuhuhisha majina ya biashara na kampuni.
Ametaja msaada wanaoutoa ni wananchi kuingiza taarifa zao kwenye mifumo mpya wa ‘mmiliki kwenye manufaa’ ambao ni kwa ajili ya kampuni zilizosajiliwa kupitia tovuti ya taasisi hiyo..
Na ATHNATH MKIRAMWENI