KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, imeridhika na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania unaoendelea mjini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa Februari14, 2022, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Joseph Mhagama, kwa niaba ya wajumbe wenzake wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama.
Amesema wamefurahishwa na kazi kubwa ambayo imekwishafanyika katika kusimamia na kuutekeleza mradi huo kwa kiwango cha hali ya juu.
Dkt. Mhagama ameongeza kuwa, kupitia mradi huo ambao unatokana na fedha zilizotolewa na Serikali inaonyesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alivyokusudia ili miguu ya Mihimili yote ya Serikali iwe pamoja mjini Dodoma.
Aidha, Kamati hiyo imeridhika na hatua zinazochukuliwa za kuzingatia usalama wa wafanyakazi wanaotekeleza kazi kwenye mradi na utoaji fursa kubwa za ajira kwa watumishi ambao ni raia wa Kitanzania.
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene, amesema maendeleo ya ujenzi huo ni kielelezo na alama kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia, imedhamiria kuhakikisha itatimiza ndoto za siku nyingi za kutaka mihimili yote ya Serikali iwe katika makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma.
Amesema mihimili mingine kama vile Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali tayari imeshahamia Dodoma na kukamilika kwa Jengo la Mahakama mihimili yote itakuwa pamoja Dodoma.
“Pongezi tunazitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuwezesha muhimili wa Mahakama kifedha ili nao uweze kuhamia Dodoma… hatua hiyo itaifanya Dodoma kuwa ‘Capital City’ ya Tanzania kwa vitendo” amesisitiza.
Wakati huo huo, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuhamia mjini Dodoma mwaka huu baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa majengo ya Mahakama.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wakati akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa majengo makubwa matatu ya Mahakama kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyotembelea mradi huo kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Amesema majengo hayo ambayo hadi kukamilika yataragharimu kiasi cha shilingi bilioni 129.7 ambazo ni fedha zinatokana na mapato ya ndani ya fedha za Serikali.
Prof. Gabriel amesema ujenzi huo ambao utakuwa na jengo la Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu (Supreme Court) upo katika hatua nzuri ambapo kazi zimekamilika kwa asilimia kubwa.
Pia, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama katika miradi mbalimbali ukiwemo huo kwa kutoa fedha kwa wakati jambo lililowafanya kasi ya ujenzi kuwa nzuri.
Kwa upande wa Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Arqes Afrika ambaye ndiye mchoraji wa ramani ya majengo hayo, Rose Nestory, amesema kuwa majengo hayo yatakuwa na Sakafu tisa na kutakuwepo na ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 300 kwa wakati mmoja.
Amesema ujenzi wa majengo hayo umezingatia sehemu ya kuendeshea shughuli za Mahakama, Ofisi za Utawala na huduma nyingine.
Rose amesema katika eneo hilo kutakuwepo na Migahawa, Uwanja wa kutua Ndege aina Helkopita , Uwanja wa kuendeshea wiki na siku ya shughuli na kujenga viwanja vya michezo na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya wadau wa Mahakama.
Na MWANDISHI WETU, Dodoma