BUNGE limesema ndani ya miezi mitatu kama Serikali haitakuja na majibu sahihi kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa Mchuchuma na Liganga litaunda Tume teule ili ilete ripoti bungeni kuhusu suala hilo kutokana na kuchukua muda mrefu kutokamilika.
Kauli hiyo imetolewa bungeni wakati wa mjadala wa mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2022/23.
“Tumechoka kusikia habari ya Mchuchuma na Liganga nashauri Serikali tuna miezi mitatu kabla ya bunge la Februari muwe mmeleta majibu, muda ukiisha kabla tutaunda kamati teule ili tulichukue wenyewe sababu ni miaka mingi imepita tunaomba suala hilo bungeni.
Jitahidini miezi mitatu ni mingi mje na majibu au tuunde kamati teule ili tuje na ripoti bungeni Ili wananchi wajue nini kinaendelea maana jambo hili ni mradi mkubwa kwa mustakabali wa nchi yetu.” Amesema Spika Job Ndugai
Akichangia mpango huo, Mbunge wa Njombe Mjini, Deo Mwanyika, ameishauri serikali kumaliza haraka majadiliano ya muda mrefu na wawekezaji katika miradi ya migodi ya makaa ya mawe na chuma ya Mchuchuma na Liganga, ili Taifa liweze kukua zaidi kiuchumi.
Amesema majadiliano ya utekelezaji wa miradi hiyo yamechukua miaka mingi, hali inayoikosesha nchi mabilioni ya shilingi pamoja na kukua kiuchumi.
Hadi sasa serikali inaendelea na mazungumzo na mwekezaji wa miradi hiyo iliyoko Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, ili kupata mwafaka wenye maslahi mapana na kuzingatia sheria za nchi katika miradi hiyo.
Miradi hiyo unganishi inajumuisha Mgodi wa Chuma Liganga wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9 kwa mwaka, kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma Liganga tani milioni 1.1 kwa mwaka, mgodi wa makaa ya mawe huko Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka.
Miradi hiyo pia inahusisha kituo cha kufua umeme huko Mchuchuma cha Megawati 600, msongo wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kati ya Mchuchuma na Liganga na Barabara kutoka Mchuchuma hadi Liganga.
Mwanyika amesema: “Majadiliano ya kuanza kwa utekelezaji wa miradi hiyo yanaendelea miaka mingi na hayaishi. Yawezekana kuna ugumu katika majadiliano, lakini tufike mahali tufikie muafaka kwani uwekezaji katika miradi hii ni muhimu katika ujenzi wa Taifa”.
Aliongeza: “Wachumi wanasema kuna gharama au kuna hasara ya kutofanya jambo fulani kwa wakati fulani. Sasa haya mazungumzo yamechukua miaka”.
Alisema hivi sasa bei ya chuma duniani imekuwa kubwa, kwamba Taifa la China pekee ndiyo wanatawala katika soko la uzalishaji wa chuma duniani.
Alisema China wanazalisha asilimia 56.5 ya chuma yote inayotumika duniani. Afrika inazalisha tani 17 lakini Tanzania inazalisha asilimia sifuri wakati chuma kipo.
“Wachina wamefanikiwa kutoa msaada duniani yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 462, kati ya hizo asilimia 80 imeenda kwenye miradi ya miundombinu, Afrika peke yetu tumepata misaada ya Dola za Marekani bilioni 106. Mnaweza kuona faida ya uzalishaji wa chuma,” alisema Mwanyika.
Alisema kuna haja kwa mpango huu kuangalia kwa mapana midai ya Mchuchuma na Liganga katika uchumi wa Taifa.
“Kama Tanzania tungeweza kuzalisha asilimia 20 ya chuma nina hakika bejeti yetu yote ingetoka kwenye biashara ya uzalishaji wa chuma.Tunone na tuna haja kila sababu haya majadiliano yanafika mwisho.”alisema.
Mwanyika alisema endapo mwekezaji anasuasua ni wakati muafaka kwa serikali kuachana naye na kutafuta mwekezaji mwingine.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Spika Ndugai, ambaye alisema suala hilo limesemwa kwa miaka mingi sana na Kwanba anasubiri kuona bajeti inayokuja kama serikali itasema chochote ili wajue watafanya nini.
“hadi leo hatujui nini kinaendelea, tumeiachia serikali muda mrefu, lakini majadiliano hayamaliziki , huenda wamekutana wanasheria tu hakuna wachumi. Tunataka kuwahi uchumi, ili nchi yetu ibadilike hapa ilipo, haya mataluma ya reli tunayojenga yangetoka kwenye chuma”.alisema.
NA SELINA MATHEW, DODOMA