WAKATI leo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatimiza miaka 45 tangu kuzaliwa kwake, Katibu Mkuu wa Chama, Daniel Chongolo, ametaja mafanikio tisa yaliyopatikana katika kipindi hicho, ikiwemo kudumisha amani, demokrasia na ukombozi wa mataifa mengine.
Ametaja sababu ya maadhimisho hayo kufanyikia mkoani Mara, kuwa ni kukumbuka na kuenzi miaka 100 ya kuzaliwa kwa mwasisi wa Chama, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Chongolo aliyasema hayo katika mjadala wa kitaifa kuhusu miaka 45 ya CCM na maendeleo ya siasa nchini, uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom.
SABABU ZA MAADHIMISHO KUWA MARA, MAFANIKIO
Akizungumzia maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Chongolo, alisema mafanikio ya Chama huanza kwa kutambua waasisi wa wake, ambao ni Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
“Hatuwezi kuzungumzia uimara wa Chama chetu hii leo bila kuzungumzia waasisi wetu Hayati Mwalimu Nyerere na Abeid Amani Karume, ambao kwa pamoja ndio waliobeba njozi au maono ya kujenga Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Alisema kwa kutambua mchango wa waasisi hao, ndiyo maana maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM yanafanyika katika Mkoa wa Mara, kwani Mwalimu Nyerere anatimiza miaka 100 tangu kuzaliwa kwake.
“Mwaka huu pia tunaadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere, ambapo ndio kusudio letu la msingi kuleta sherehe huku za miaka 45 ya Chama chetu mkoani Mara,” alisema.
Alieleza katika kipindi cha miaka 45, Chama kimefanikiwa kudumisha amani, akibainisha kwamba kwa kipindi chote hicho hakuna jambo lililoleta dhoruba kwa nchi.
Chongolo alisema eneo jingine ambalo Chama kimepiga hatua ni kujenga demokrasia ya pekee isiyofanana na taifa lolote duniani na kwamba inajipambanua.
“Hili linajidhihirisha wakati wa kubadilishana madaraka, tumeona mabadiliko yametokea hakuna kuangaliana kwa husda wala nini mambo yanakwenda vyema,” alisema.
Aliyataja mambo ambayo CCM kinajivunia ni kuwa mkombozi wa mataifa hasa ya Kusini mwa Afrika, ambapo ilihakikisha nchi hizo zinakuwa huru.
“Chama cha Mapinduzi kinajivunia kuwa ni Chama cha ukombozi na hasa kwa mataifa kusini mwa Afrika, kupitia CCM na serikali sisi ndio tumewasaidia wengine wote waliokuwa na changamoto kwenye mataifa yao,” alisema.
Aliyataja mafanikio mengine ni kulifanya taifa kuwa moja bila kubaguana kikabila wala jinsia, kusimamia matumizi ya rasilimali za nchi kwa ajili ya wote, ujirani mwema na mataifa ya nje na katika hilo, Tanzania imekuwa ikisuluhisha migogoro mingi ya mataifa mengine.
Katibu Mkuu Chongolo alifafanua kwamba, Chama kinajivunia kusimamia mageuzi ya mfumo wa ndani kuendana na wakati na hata uteuzi wa viongozi wa CCM unazingatia nani anateuliwa ili afanye nini.
Alitaja mafanikio mengine ni katika utekelezaji wa miradi ya huduma kwa wananchi ikiwemo afya, elimu, miundombinu na mambo mengine lukuki chini ya awamu mbalimbali za serikali.
MZEE CHISSANO
Akitoa salamu za pongezi wa CCM kwa kutimiza miaka hiyo, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquima Chissano, alisema ni ngumu kukumbuka mwanzo wa Chama bila kuvikumbuka ASP, TANU na viongozi wake ambao ni Mwalimu Nyerere na Karume.
“Ninashukuru kualikwa kwenye mkutano huu wa kuadhimisha miaka 45 iliyopita ya CCM, lakini pia huwezi kukumbuka miaka 45 bila kukumbuka Afro-Shirazi Party, TANU na viongozi kama Mwalimu Nyerere na Karume,” alisema.
Alibainisha kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo unaopaswa kuwa mfano kwa muungano wowote Afrika kwa kuwa ndiyo imara zaidi kuliko wowote ule.
“Mimi nilikuwa hapo nimeona maendeleo baada ya Uhuru tumekaa miaka michache bila kutembelea Tanzania nilipotembelea nilishangaa maendeleo, sio magorofa pekee bali watu wenyewe,” alisema.
Alitofautisha vijana wa sasa na wale kabla ya miaka 45, akisema wamebadilika kutokana na kuelimika na kusisitiza mabadiliko ya miji, miundombinu ya barabara na madaraja.
“Vijana wa Tanzania wa sasa sio kama wale wa miaka 45 iliyopita kuna tofauti kubwa sana, Nyerere alikuwa mmoja wa wale walioleta umoja wa vyama vya kupigania uhuru wa Msumbiji,” alisema.
Alieleza yeye ni miongoni mwa wananchi waliolazimika kusubiri siku mbili ama tatu Rufiji, ili kuvuka kwenda upande mwingine na hilo lilitokana na ubovu wa miundombinu kwa wakati huo, lakini sasa halipo tena.
“Mimi ni mshirika kidogo katika kusomesha watu kufanya kazi kwa mikono yao, mtu ajue kufanya kitu ikiwemo kujenga na hii mifano ipo Tanzania,” alisema.
Aliipongeza CCM na Watanzania kwa ujumla kwa kazi wanayofanya na namna ilivyoisaidia Msumbiji katika ukombozi wake.
Alieleza CCM na Tanzania kwa ujumla imekuwa ikiendelea kutoa msaada kwa taifa hata wakati huu, ambapo taifa lake linakabiliwa na changamoto za ugaidi.
“Tunasema asanteni sana endeleeni na kazi CCM endelea kuongoza muwe mfano, Nyerere alikuwa mmoja wa waliosaidia umoja wa kupigania Uhuru wa Msumbiji,” alisema.
MABODI
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Juma Abdallah ‘Mabodi’, alisema maridhiano ya Zanzibar yamekuwa chachu ya mshikamano na ushirikiano miongoni mwa Wazanzibari na hayo yanatokana na sera bora zilizowekwa na CCM kwa kipindi hicho.
Alieleza jambo jingine linalofanywa na CCM ni kugawana manufaa ya nchi bila kujali itikadi, jambo ambalo limekisaidia Chama kuendelea kuaminika.
Mabodi alibainisha jambo jingine muhimu kwa Chama ni usikivu wake hata kwa vyama vya upinzani vinaposhauri, kinaangalia kama kuna tija kwa taifa na kufanyia kazi.
“Baada ya vyama vingi kuanzishwa kulitokea mifarakano baina ya vyama hivyo lakini sifa kuu tuliyonayo hakuna msuluhishi yeyote aliyetoka nje aliyekuja kusuluhisha mifarakano hii, hivyo tuliweza kukaa pamoja na kuridhiana kwa pamoja na mpaka sasa nchi iko shwali,” alisema.
KANALI LUBINGA
Naye, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga, alisema msingi wa mafanikio ya CCM ni mwenendo mzuri uliofanywa na TANU na ASP.
Lubinga alieleza zamani kulikuwa na mambo ya kimkakati na msingi ya kuimarisha uhuru, amani na utulivu na hayo yalifanikiwa kutokana na ilani bora zinazotengenezwa kuendana na mahitaji ya wananchi ya wakati husika.
Alisema jambo jingine ambalo CCM imefanya ni kujenga uhusiano wake na vyama vingine nje ya Tanzania, vikiwemo rafiki na vyama ndugu ambavyo ilishirikiana navyo katika ukombozi.
Kanali mstaafu Lubinga, aliongeza kwamba Chama kimekuwa kikijiimarisha katika shughuli zote hizo ili kuwaletea wananchi maendeleo na ndiyo maana leo hii watanzania wa kila mkoa wanazungumza lugha moja.
Alisisitiza matumizi mazuri ya rasilimali na umakini wa watendaji kwa kila kilichopo, umeendelea kukipa heshima Chama hadi leo tangu miaka 45 iliyopita.
“Leo hii tumempoteza Hayati Rais Magufuli na ameingia Rais Samia, lakini hakukuwa na changamoto yoyote kwa wenzetu hiyo ingekuwa hali ya hatari, tunakipongeza sana hiki Chama,” alisema.
MWAKILISHI WA ANC
Mwakilishi kutoka Chama cha ANC cha Afrika Kusini, Ndumi Gwayi, alisema CCM kimeonyesha umahiri mkubwa katika uongozi na hilo linajidhihirisha kwa kuwa na Mwenyekiti mwanamke.
Gwayi alieleza Chama hicho kimekuwa msingi mkubwa wa ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika na kilisisitiza umuhimu wa Waafrika kujitegemea kama sehemu ya dhamira ya kuanzishwa kwake.
MWAKILISHI WA SWAPO
Katibu wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama cha SWAPO cha Namibia, Katrina Liswani, alipongeza hatua ya CCM kutimiza miaka 45 huku kikiwa na uongozi wa mwanamke.
Liswani alisema kupitia CCM wamejifunza kutekeleza sera ya ujamaa na kujitegemea na zimewafanikishia kuwa na maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa zamani.
“Hatutasahau mambo mliyotufanyia, ikiwemo kuwasomesha watu wetu na mambo mengi tumeyapata huko, tunajivunia hayo sana asanteni sana kaka na dada zetu,” alisema.
BALOZI PEREILA
Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Pereila Silima, alisema, “CCM kimepeleka walinda amani wengi nje ya nchi lengo ni kuhakikisha amani inadumu na lengo la kuwakomboa wengine halitatimia iwapo hawatakuwa na amani,” alisema.
Alisema kazi kubwa ya CCM tangu mwanzo haikuwa kuwakomboa wananchi kupata uhuru pekee, bali ni kuhakikisha wanaongeza vipato vyao na sasa imeshuhudiwa serikali ikishirikiana na mataifa mbalimbali katika uwekezaji ili kulifanikisha hilo.
Balozi Pereila alieleza kupitia sera za kimataifa, wanahakikisha kwamba Chama kinakuwa mkombozi wa mataifa mengine ya Afrika.
“CCM inahitajika ilivyo na ikiwa imara zaidi ili kutekeleza malengo yote ya kuimarisha Bara la Afrika,” alisema.
WASSIRA
Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wassira, alisema CCM kilipoanzishwa kilirithi mfumo wa maadili kutoka ASP na TANU na kwamba, msisitizo wa maadili haukuwahi kubadilika ila muundo wa kuenenda maadili ndiyo unajibadilisha kila wakati.
Wassira alieleza mafanikio ya CCM yametokana na misingi ya maadili ambayo huwapa miongozo ya nini viongozi wafanye na nini wasifanye kwa kuzingatia Chama ni taasisi kubwa.
“Miaka ya 1980 kwa sababu zinazoeleweka na mabadiliko ni lazima miiko ya viongozi iliondolewa na watu walidhani CCM imeacha ujamaa, jambo ambalo sio kweli kwa sababu katika Katiba yetu hadi ya leo sera yetu ni ya kijamaa,” alisema.
Alieleza kwa sasa CCM imeunda idara maalumu ya maadili ambayo kimsingi ina jukumu la kusimamia maadili ya wanachama wake.
KIHONGOSI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Kenani Kihongosi, aliahidi kuwa bega kwa bega na Rais Samia na kusisitiza kwamba, watahakikisha heshima yake inalindwa wakati wote.
Kihongosi alifafanua katika miaka 45 tangu kuzaliwa kwa CCM, kundi la vijana limekuwa na nafasi kubwa ya ujenzi wa Chama na nchi ili kuleta maendeleo.
“Nafasi ya Umoja wa vijana katika Chama cha Mapinduzi kuelekea miaka 45 imeonekana katika nyanja mbalimbali, zikiwemo za kiuchumi, maendeleo na una nafasi kubwa hasa kwa Chama kujisahihisha kwa wananchi na kuleta maendeleo katika taifa letu,” alisema.
Aliongeza kwamba hata historia inaonyesha kwamba kuzaliwa kwa CCM kwa maana muungano wa ASP na TANU ulihusisha juhudi za vijana katika kulifanikisha hilo.
“Nafasi ya vijana katika Chama imeonekana katika nyanja mbalimbali kwa miaka hii 45, viongozi wengi wa taifa letu hii leo wamepita katika UVCCM na hiyo inaonyesha namna gani jumuiya hii ina mchango mkubwa katika kushajihisha viongozi,” alisema.
Alieleza pia serikali ya CCM imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo sehemu kubwa ya wafanyakazi ni vijana huku Vyuo vya Ufundi vikiendelea kujengwa, ili kuwafundisha vijana ufundi mbalimbali ili wajiajiri.
“Mambo mengi mazuri makubwa yamefanywa kwa sababu ya nguvu kazi ya vijana, unapoongelea miradi mikubwa ya maendeleo vijana wamefanya kazi kubwa kuhakikisha miradi hiyo wanatoa nguvu kazi na inaweza kujengeka,” alisema.
KATE KAMBA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba, alisema mafanikio makubwa yaliyotokana na Chama yanahusisha mchango wa Jumuiya ya Wanawake (UWT).
Alieleza jumuiya hiyo ndiyo husimama kidete kutetea viongozi na wagombea wa Chama kuhakikisha wanashinda uchaguzi na ndiyo iliyobeba wanawake kadhaa leo hii wanashika hatamu ndani ya serikali.
“Jumuiya ya wanawake ni muhimu sana katika Chama chochote kwani ndio wanaobeba jukumu kubwa la kulea Chama, hivyo Jumuiya yetu ya Wanawake CCM imedumu kwa muda wote tangu kuanzishwa,” alisema.
NA JUMA ISSIHAKA