KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema kuwa, Chama kitasimama imara kuwa wakili wa kusemea, kupigania na kutetea haki na stahiki za wazee nchini.
Pia, amesema CCM itapigania kuboreshwa kwa upatikanaji wa mafao ya wastaafu, wazee kuwekewa utaratibu bora wa kisheria wa huduma za afya na kupata uwakilishi katika vyombo vya uwakilishi, ikiwemo kuwakilishwa ndani ya Bunge na mabaraza ya madiwani.
Chongolo aliyasema hayo, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, alipokuwa akizungumza na Baraza la Wazee wa Wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, katika mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma, Katavi na Tabora, kukagua uhai na uimara wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025.
“Nakubaliana na ninyi kuwa Sera ya Wazee ya Mwaka 2003 ni nzuri sana lakini imechukua muda mrefu kuwa sheria. Kwa namna hali inavyokwenda kwa sasa katika jamii yetu ni bora tukafikiria kwenda mbele zaidi.
Tuwe na sheria itakayolinda haki za wazee na kuelezea wajibu wa watoto kwa wazazi wao. Tuna sheria hapa inakutaka wewe mzazi kuwajibika kwa mtoto kuhakikisha anapata haki zake. Lakini wapo watoto wanaowatelekeza wazazi wao wakiwa wamezeeka.”

“Kwa namna ile ile ambayo tulitunga sheria ambayo inawawajibisha wazazi basi tuwe na sheria inayowawajibisha watoto kuwatunza wazee wao badala ya kuwasahau.
Katika hili la sheria ya kulinda haki za wazee na wajibu wa watoto kwenu nitakuwa wakili wenu namba moja. Juzi nililisema hili pia nilipokutana na Wazee wa Chato, nilikutana nalo pia nilipozungumza na Wazee wa Muleba huko Kagera,” amesema Chongolo.
Akizungumzia kuhusu wazee kuwakilishwa katika vyombo vya uwakilishi, ikiwa ni pamoja na bunge, Chongolo alisema kuwa kundi hilo maalum katika jamii linastahili kuwekewa utaratibu huo, akisistiza kuwa iwapo mchakato wa kiserikali utachukua muda mrefu, CCM inaweza kuweka suala hilo kupitia taratibu za ndani ya chama, kama ambavyo makundi mbalimbali mengine, ikiwemo wanawake, watu wenye ulemavu, vijana na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, yana uwakilishi bungeni.

Chongolo aliwaambia waze hao kuwa kupitia utaratibu wa kisheria unaoandaliwa na Serikali kuwasilisha mswada wa Bima ya Afya kwa wote, itakuwa ni mojawapo ya fursa nzuri kuhakikisha kundi la wazee linapata huduma za afya kwa uhakika, kwa sababu katika umri wao wa uzeeni, matibabu ya magonjwa mbalimbali yanayowasumbua uzeeni, ni mojawapo ya huduma za msingi baada ya kulitumikia taifa kwa mafanikio.
Kwa upande wao, wabunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako na Jimbo la Kasulu Vijijini, Agustino Vuma, wakizungumzia changamoto mbalimbali ambazo bado Serikali ya CCM inazifanyia kazi, walisema, kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na barabara, walitumia nafasi hiyo kuwasemea wananchi kuhusu mahitaji ya umeme na maji katika maeneo hayo.
“Ndugu Katibu Mkuu wa CCM, tunashukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imeendelea kushusha fedha kwa ajili ya miradi ya barabara ambayo zinaufungua mkoa na wilaya za Kigoma kutuunganisha na maeneo mengine kwa kasi kubwa.

Mwaka huu hakutakuwepo na kero ya kuwachangisha wazazi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa…serikali imeshusha fedha za kutosha. Changamoto kubwa ni upatikanaji wa maji safi, salama ya kutosha na usambazaji wa umeme wa REA awamu ya tatu, ambazo nazo zinaendelea kufanyiwa kazi kwa mipango iliyoko katika bajeti,” alisema Profesa Ndalichako.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Kijijini Vuma Agustino mbali ya kuelezea namna ambavyo Serikali imetenga na kushusha fedha za bajeti za maendeleo ya huduma za afya, barabara na elimu, pia aliwasemea wananchi kuhusu kero ya mgogoro wa ardhi katika Msitu wa Kagerankanda, ambapo wananchi wanahitaji kuwekewa mipaka kwa ajili ya matumizi sahihi ya ardhi hiyo, hususan kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Na MWANDISHI WETU, Kigoma