KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema CCM itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu na Chama cha Ukombozi cha Msumbiji (FRELIMO), ili kuenzi ushirikiano wa kihistoria ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo.
Aliyasema hayo Dar es Salaam, wakati akimkaribisha Katibu Mkuu wa FRELIMO, Roque Samuel, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya vyama hivyo.
Chongolo amesema CCM chini ya uongozoi wa Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, itaendeleza ushirikiano wa kindugu kwa nguvu zote, kwani Tanzania na Msumbiji ni kama kaka na dada ambapo undugu wao hauwezi kutenganishwa.
“Undugu wa CCM na FRELIMO ni wa kihistoria, ulioanza toka harakati za mapambano ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, ukiongozwa na waasisi wetu, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mwasisi wa FRELIMO, Eduardo Mondlane na Rais Samora Machel,” alieleza Chongolo.
Chongolo alifafanua kuwa, CCM inawajibu wa kuendeleza na kudumisha ushirikiano huo ili uendelee kuishi.
“Uendelee kuishi katika kizazi hiki tulichopewa dhamana ya kuongoza na katika kizazi kijacho ambacho tutakiachia jukumu la kuongoza nchi zetu,” alisema.
Alibainisha ushirikiano huo utajikita katika sekta za uchumi na kijamii ambapo kazi kubwa ni kuimarisha uchumi wa mataifa hayo ili kuwa na siasa endelevu.
“Bila kuwa na uchumi imara, kuna shida na ni lazima tuendelee kujenga muhimili huu wa uchumi katika mataifa yetu, huku tukishirikiana na tukishikamana ili kuleta matokeo ya kuwa na mataifa yenye utulivu katika uongozi wetu na kizazi kijacho,” alieleza Chongolo.
TISHIO LA UGAIDI
Alisema mataifa hayo kwa sasa yananyemelewa na vitendo vya ugaidi ambavyo vinahatarisha amani na utilivu, pamoja na uchumi imara.
“Niseme tu tusikate tamaa. Lazima tuendelee kushirikiana na kushikamana na kuongeza mapambano dhidi ya magaidi hawa, kwa sababu tukiwa pamoja na nguvu ya kupambana nao itakuwa kubwa, lakini tukiacha kila mmoja kivyake nguvu itapungua, hivyo wao wataweza kutushinda kirahisi,” aliieleza.
Alisema, CCM inafahamu tishio la ugaidi nchini Msumbiji, hasa katika Jimbo la Cabo Delgado.
Alisema, jimbo hilo liko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji hivyo Tanzania ni mwathirika wa ugaidi huo
“Serikali ya CCM inawahakikishia kuwapa kila namna ya ushirikiano kuhakikisha hilo jambo linatokomezwa kwenu na sisi tuendelee kuwa salama,” alisema.
Pia, Chongolo alisema ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha Pwani, umekamilika na kinasubiri makubaliano baina ya makatibu wakuu na wenye viti kutoka vyama vya mataifa sita ya Kusini mwa Afrika yaliyokubaliana kukijenga.
“Ni chuo muhimu kutujengea msingi wa umoja na kurithisha historia kwa vizazi vijavyo,” alisema.
FRELIMO
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa FRELIMO, Roque Samuel, alisema ziara hiyo inalenga kuimrisha ushirikiano wa vyama na serikali.
“FRELIMOI iko tayari kushirikiana na CCM kwa hali na mali. Tunaiona Tanzania kama mbia ambaye hatutapenda kumpoteza,” alisema Samuel.
Alisema ushirikiano huo uendelee pia katika kukomesha matishio ya ugaidi unaondelea Msumbiji ambao una athari pia kwa upande wa Tanzania.
“Tunatakiwa kulliona tatizo hili katika upana, kwamba nyuma yake wale maadui zetu ambao wanafanya jitihada za kuviondoa vyama tawala ndiyo walio nyuma ya ugaidi huu,” alisema.
Alisema nchini humo hadi sasa watu 700, wamuawa na magaidi ambao wanauwa bila kujali watoto na wanawake.
“Watu 180,000 hawana makazi. Nyumba zilivunjwa, zikachomwa moto,” alisema.
Na CHRISTOPHER LISSA