CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakitosita kuiagiza serikali kuvunja mikataba ya wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.
Aidha, kimewataka wanachama kujibu hoja zinazotolewa na watu wanaopinga kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, badala ya kukaa kimya dhidi ya upotoshaji unaofanywa na watu hao.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Christina Mndeme, wakati akikagua ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ya Mlele.
“Sijaridhishwa na kazi ya mkandarasi mshauri kampuni ya BICCO. Hajatekeleza majukumu yake ya kulinda fedha za serikali zinazotumika katika ujenzi huu.
Aliongeza kuwa: “Chama kinaagiza mradi huu ukamilike kwa wakati na hakitosita kuishauri serikali kuvunja mkataba kama mkandarasi anafanyakazi zake kwa kusuasua.”
Christina alimuagiza mkandarasi anayejenga jengo hilo kampuni ya SUMA JKT, kuongeza kasi ya ujenzi kwa kuleta nguvu kazi ya kutosha.
Kadhalika, aliuagiza uongozi wa halmashauri kuandaa taarifa yenye usahihi kuhusu kiasi halisi cha fedha kilichotumika katika mradi huo, baada ya kubaini ukakasi katika takwimu za fedha zilizotengwa.
“Mradi huu mmenieleza unagharimu sh. bilioni 2.8, mkataba mpya na SUMA JKT unagharimu sh. bilioni 2.1, mmelipa mkandarasi TBA sh. milioni 499 ambaye mkataba wake umevunjwa.
“Lakini hapa kuna sh. bilioni moja ambazo halmashauri imetenga kwa ajili ya mradi huu, nataka kujua hizi fedha matumizi yake ni yapi? Hizi ni fedha za serikali, hivyo lazima matumizi yake yafahamike,” alisisitiza.
Kufuatia kukosekana majibu ya maswali hayo, kiongozi huyo aliagiza kuandaliwa taarifa yenye usahihi wa matumizi ya fedha halisi za mradi huo, ambao tangu mwaka wa fedha 2016/2017 hadi sasa bado haujakamilika.
Aidha, aliwataka wakandarasi washauri kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya nchi badala ya kufumbia macho vitendo vinavyoashiria miradi ya ujenzi kwenda kinyume cha matakwa ya kimkataba.
Katika hatua nyingine, akiwa katika mkutano wa Shina Namba 6, Kata ya Utende, Christina, aliwataka wanachama wa CCM kujibu hoja zinazotolewa na watu wanaopinga kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayofanywa na Rais Samia.
Alisema Rais Samia anafanya kazi nzuri ya kuhakikisha maendeleo ya haraka yanawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ni jukumu letu kujibu hoja za watu wanaopinga mazuri yanayofanywa na Rais Samia, badala ya kukaa kimya,” alieleza.
Pia, alisema sekretarieti mpya ya CCM inaendelea kuimarisha Chama kuanzia ngazi ya mashina, kuongeza hamasa ya wananchi kujiunga na Chama na kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mlele (CCM), Mhandisi Issack Kamwelwe, alisema vijiji vyote vya jimbo hilo vina zahanati, huku mradi mkubwa wa maji ukiwa ukingoni kukamilika.
Alisema hali ya upatikanaji nishati ya umeme imeendelea kukamilika na hivi karibuni wilaya hiyo itaunganishwa na gridi ya taifa.
“Kwetu sisi utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ni kwa vitendo na si maneno,” alieleza mbunge huyo.
Na MUSSA YUSUPH, Mlele