KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema Chama hicho sio cha chaguzi, chokochoko, maneno na fitina, hivyo wasiokubali kushindwa waache wabunge na waliopewa dhamana wafanye kazi.
Amesema CCM, hakitahangaika na wanaotafuta nafasi za uongozi kwa nguvu bali itatumia mifumo kuwashughulikia, kwakuwa kina jukumu kubwa la kumsaidia Rais Samia Suluh Hassan kusimamia miradi ya maendeleo.
Amewataka wanaotunisha misuli na kulewa madaraka kujishusha na kuimarisha uhusiano, ili kutoleta majeraha uchaguzi wa 2025.
Pia amesisitiza umuhimu wa sensa na kuwataka viongozi wa CCM, kuhakikisha wanazungumzia suala hilo kila sehemu kwakuwa ndiyo itaayofanikisha mipango ya maendeleo.
Katibu Mkuu Chongolo, amesema hayo ya kupokelewa Mkoani Lindi, katika ziara ya kuhamasisha uhai wa Chama kwa umma na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025.
Amesema CCM , haiwezi kuwa Chama cha uchaguzi, maneno, fitina na chokochoko kila siku kwakuwa kutoa nafasi ya vitu hivyo ni kujidhoofisha wenyewe.
“Tumekuja kufanya kazi za Chama tupo hapa tumetumwa na Rais Samia, ndiye mwenye Chama, tumefanya mapitio kabla ya kuja hapa kuna changamoto kuna tatizo la uhusiano, mnagombea nini uchaguzi umeisha? waacheni wabunge wafanye kazi,”amesema.
Chongolo amesema, chokochoko zilizopo kwenye majimbo zikiendelea Chama kitaingia kwenye uchaguzi 2025 kikiwa na majeraha.
Na MARIAM MZIWANDA