CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza rasmi mchakato wa uchukuaji wa fomu za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya aliyekuwa Spika wa wa Bunge hilo, Job Ndugai kujiuzulu Januari 6, mwaka huu.
Akizungumza, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika Ofisi Kuu za CCM Zanzibar, Kisiwandui alisema Ndugai aliandika barua kwa hiari yake na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma, hivyo chama kinawatangazia wanachama wote kuanza mchakato wa kujaza nafasi hiyo.
Katibu huyo alisema kuanzia Januari 10 hadi 15, mwaka huu mchakato wa uchukuaji wa fomu na urejeshaji utaanza na kwamba kwa wanachama ambao wana sifa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya CCM, wanakaribishwa kuchukua fomu katika ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma, Ofisi Ndogo Lumumba na Ofisi Kuu Zanzibar Kisiwandui.
“Idara ya Oganaizesheni ya CCM ndio waratibu wa mchakato huu, hivyo wanachama wanaotaka kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hii wakifika ofisi za CCM ambazo zitakuwa zikitoa fomu watapewa maelekezo,”alisema.
Shaka alisema Januari 17, mwaka huu Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM itakutana kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu wagombea ambao wamejitokeza kugombea nafasi hiyo.
Alisema Januari 18 hadi 19, mwaka huu watachuja majina ya wagombea wa nafasi hiyo na kufanya uteuzi wa mwisho, ambapo Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itafanya kazi hiyo na hatimaye Januari 21 hadi 30, mwaka huu kokasi ya wabunge wa CCM itakutana kupiga kura ili kumpata mgombea.
Shaka alisema baada ya kokasi kupiga kura ya wagombea hao na kumpata mgombea ambaye atakwenda kusimama Bungeni kwa ajili ya kuomba kuchaguliwa kuomba kuwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mchakato huo utakamilishwa na kokasi ya wabunge wa CCM.
“Kwa nafasi hiyo CCM inawatangazia wanachama wake wote kuwa utaratibu wa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea atakayechaguliwa na wabunge wa Bunge hilo ya kujaza nafasi ya Spika na utaratibu huu ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayotambua Spika ndiyo kiongozi mkuu wa Bunge, kwa hiyo nafasi hiyo haiwezi kuwa wazi na bunge kuendelea na shughuli zake,”alisema.
Alisema kama inavyoeleza katika Katiba ibara ya 84 kifungu kidogo cha kwanza, ambapo kutakuwa na Spika ambaye atachaguliwa na wabunge kutoka kwa watu ambao miongoni mwao ni wabunge au kwa watu ambao wenye sifa ya kuwa wabunge, atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine nje ya Bunge.
Shaka alisema katika ibara ya 84 kifungu kidogo cha nane katika Katiba hiyo inaeleza hakutakuwa na shughuli yeyote ambayo itakayotekelezwa katika Bunge isipokuwa uchaguzi wa Spika wakati wowote ambao kiti cha Spika kitakuwa kipo wazi.
“Lakini ibara ya 86 kifungu kidogo cha kwanza inaeleza kutakuwa na uchaguzi wa Spika katika kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya na katika kikao chochote mara baada ya nafasi ya kiti cha spika kikiwa kiko wazi, hivyo katika kutekeleza matakwa ya Katiba CCM inatangaza kuanza mchakato wa utoaji wa fomu katika kujaza nafasi hiyo,”alisema.
NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR