CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemtembelea na kumjulia hali Mzee Rehan Waikela, aliyelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), kwa matibabu.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, juzi alimtembelea Mzee Waikela katika taasisi hiyo, iliyoko Jijini Dar es Salaam.
“Chama Cha Mapinduzi na serikali zake kinathamini na kujali kila mtu aliyejitoa na kujitolea kwa hali, mali, vitu, ujuzi na maarifa kufanikisha uhuru wa nchi yetu na ukombozi wa Afrika.”
“Mchango wao haupimiki wala hauwezi kuthaminishwa kwa chochote bali kwa kuwatambua, kuwajali na kuwatunza inaweza kuwa namna bora zaidi ya kutambua mchango wao,” alisema.
Mzee Waikela amekuwa mmoja kati ya viongozi wa Chama cha TANU wakati huo ambaye alijitoa na kujitolea kwa hali na mali kuwapa ushirikiano wapigania Uhuru ili kufanikisha lengo hilo.
Historia inamtaja kuwa wakati viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, walipokuwa wakifika mkoani Tabora, Mzee Waikela alikuwa akiwalaki kwa malazi, chakula na kuwapa huduma ya usafiri ili kuhamasisha harakati za Uhuru na Ujenzi wa Chama cha TANU wakati huo.
NA MWANDISHI WETU