CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemuomba radhi Mwenyekiti wake ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amirijeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan, kutokana upotoshwaji wa taarifa iliyochapishwa leo na Gazeti la Uhuru toleo No. 24084.
Upotoshwaji huo ulifanywa na Gazeti la Uhuru likimnukuu Rais Samia katika mahojiano yake na Salim Kikeke, Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), katika Ikulu ya Dar es Salaam.
Kutokana na hatua hiyo Bodi ya Uhuru Media Group (UMG), imewasimamisha kazi kupisha uchunguzi, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Ernest Sungura, Naibu Mhariri Mtendaji, Ramadhan Mbwaduke na Mhariri wa zamu wa gazeti hilo Rashid Zahoro.
Pia, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amesimamisha uchapishaji wa Gazeti hilo kwa siku saba kuanzia leo, Agosti 11.
Akizungumza na waandishi wa habari, katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam, amesema Gazeti la Uhuru ni mali ya CCM, hivyo litawajibishwa kwa utaratibu wa ndani ya Chama.
“Hatuwezi kulikana hili ni Gazeti letu na limekosea kwa kumlisha maneno Rais, niliagiza Bodi ikae, imefanya hivyo mara moja na imechukua hatua,” amesema Chongolo.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwaonya viongozi na wanaCCM wanaopingana na maagizo ya Chama.
“Hakuna mtu aliye juu ya Chama hiki, atakayekwenda kinyume chama kina mifumo ya kumshughulika, hata mimi umewekwa utaratibu namna ya kushughulikiwa hivyo niwaonye viongozi wanaoona wao wako juu na kupinga maagizo au matamko ya viongozi wakuu, hatutawaacha.”