CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesifu hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan, kujali na kuwasilikiza wananchi kwa kushughulikia malalamiko yaliyotokana na tozo za miamala ya simu, kikimtaja kuwa na msimamo imara na thabiti.
Kimesema punguzo la tozo hizo ni unafuu kwa wananchi, ambao idadi kubwa wamekuwa wakitumia miamala ya simu kuendesha shughuli za kiuchumi na kusaidia wahitaji.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, wakati akizungumza na vijana wa taasisi ya mama yangu, nchi yangu inayoshughulika na uhamasishaji vijana.
Shaka alisema uamuzi huo umetolewa wakati mwafaka na kusisitiza kuwa pamoja na punguzo hilo, wananchi wanapaswa kufahamu wana wajibu wa moja kwa moja kuchangia maendeleo ya ujenzi wa taifa. Shaka alisema kitendo kilichofanywa na serikali chini ya Rais Samia, kimeonyesha uzalendo na uungwana kwa kuwajali na kuwasikiliza wananchi wake.
“CCM inampongeza Rais Samia kuwasikiliza wananchi kuhusu sakata la tozo za miamala ya simu, ambapo alitoa maelekezo ya viwango hivyo kutazamwa upya na sasa imepunguzwa kwa asilimia 30 huku kampuni zikipunguza kwa asilimia 10.
“Kazi ya kujenga nchi ni wajibu wa Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa. Uamuzi huu ni upendo mkubwa alionao kwa wananchi anaowaongoza ili washiriki kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa furaha,” alisema Shaka.
Hata hivyo, alibainisha wananchi wanapaswa kuelewa ni jukumu la kila mmoja kushiriki kazi ya ujenzi wa nchi na kuweka msukumo wa maendeleo na kupeleka huduma za jamii katika maeneo yote.
Aliwataka watendaji wa serikali kutambua kuwa kazi ya kumsadia Rais Samia katika kila eneo ni wajibu usiohitaji kuelelezwa wala kusukumwa, badala yake wautimize ipasavyo wakiweka mbele maslahi ya umma.
Shaka aliwataka Watanzania kupuuza uvumi unaoenezwa mitaani kuwa serikali ina mpango wa kusitisha elimu bila ada.
“Serikali ya Rais Samia itaendelea kugharamia elimu bila ada kwani unawagusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi.
Zaidi itaendelea kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili mpango huu ili wanafunzi wa Tanzania wapate elimu katika mazingira mazuri zaidi. Hivyo niwaombe wananchi wapuuze taarifa zinazodai serikali itausitisha,” alisema.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kundi hilo, Agness Maganga, alieleza kuwa wanamuunga mkono Rais Samia kwa kuwa serikali anayoiongoza imefanya mambo makubwa yakiwemo kupandisha madaraja watumishi wa umma 92000.
Pia kuondoa tozo ya asilimia sita ya kulinda thamani ya mkopo kwa wanufaika wa mkopo elimu ya juu, kuongeza bajeti ya mikopo elimu ya juu na kuendelea kutoa fedha kukamilisha na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati nchini.

KAULI ZA WATOA HUDUMA ZA SIMU
Akizungumza na UHURU, Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Mitandao ya Simu Tanzania (TAMNOA), Hisham Hendi, alipongeza hatua ya serikali kufanya mazungumzo nao kujadili mbinu za haraka na muda mrefu katika ufanikishwaji wa azma ya serikali ya kuanzisha tozo ya mshikamano.
“Tunaipongeza serikali kupitia Wizara ya Fedha na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kufanya mazungumzo kadhaa na tasnia hii kujadili mbinu za haraka na za muda mrefu ili kufanikisha azma ya serikali kuanzisha tozo ya mshikamano na kujadili kwa upana ustawi wa sekta hii,” alisema.
Pia aliipongeza serikali kupunguza asilimia 30 ya tozo hiyo, huku wao wakiwa wamepunguza asilimia 10 na kuongeza kuwa, ni imani yao kuwa hatua hiyo zitarudisha wateja walioacha kutumia huduma hiyo au kufanya biashara.
Hendi ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom, alibainisha kuwa katika katika enzi ya 4IR, sekta ya mawasiliano ina jukumu la kuziwezesha nyingine, zikiwemo ‘agritech’, ‘telemedicine’, malipo ya serikali na huduma katika kuendelea kuchangia ukuaji wa Taifa.
“Wanachama wa TAMNOA wamejitolea kuendelea kuwekeza katika ubunifu na uvumbuzi mpya lakini ili kufikia huko ni muhimu tuendelee kupata faida,” alisema.
Alisisitiza kuwa, ni muhimu kwa wadau wa sekta hiyo kufanya kazi kwa karibu na serikali, ili kujengeana maarifa juu ya ukusanyaji ushuru kupitia majukwaa ya kidigitali yanayofanya kazi kwa karibu na wadhibiti na wadau wengine kuhakikisha kufikiwa kwa malengo kwa usawa kati ya sekta binafsi na umma.
Na JUMA ISSIHAKA