KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeridhia na kuunga mkono hatua ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, kufanya majadiliano na viongozi wa vyama vya siasa yenye lengo la kufikia maridhiano ya demokrasia kwa maslahi ya taifa.
Pia, CCM imesisitiza kuendeleza majadiliano hayo kwa dhumuni la kujenga jamii yenye usawa, uhuru wa kujieleza na kushiriki shughuli za kisiasa kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema Kamati Kuu ya CCM iliyoketi Mei 22, 2022, ilikutana kwa ajili ya kupokea, kisha kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa.
“Kamati Kuu ilijadili masuala ya mbalimbali ya kitaifa ikiwemo hatua zinazochukuliwa na Rais Samia katika kujenga maridhiano ya kisiasa.
Aliongeza kuwa: “Kamati Kuu imempongeza na kumuunga mkono Rais Samia kwa hatua anazoendelea kuchukua, kukutana na kufanya mazungumzo na makundi ya kijamii katika kujenga amani, haki na maridhiano.”
Shaka amesema Kamati Kuu ya CCM, imetambua na kuridhia dhamira ya dhati ya Rais Samia kufanya maridhiano kwa kuzingatia uendelezaji urithi, tunu na msingi imara wa ujenzi wa taifa, kuviwezesha vizazi vijavyo virithi taifa jema lililo imara.
Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi, amesema Chama kinatambua mazingira na mahitaji ya kisisa yaliyopo ndani ya jamii, hivyo kufanikiwa kwa majadiliano hayo, kutawanufaisha wananchi katika kuimarisha misingi ya utawala bora na utoaji huduma za kijamii.
“CCM ndicho chama kiongozi na kikomavu katika siasa za nchi, kipo tayari kuendeleza mjadala wenye lengo la kuimarisha demokrasia endelevu kwa maslahi ya taifa,” alisisitiza.
Shaka ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia, kwani amekuwa kiongozi mwenye kuliunganisha taifa.
HISTORIA YA MARIDHIANO
Shaka alisema CCM ndicho chama kiongozi ambacho kimekuwa kikitoa mwelekeo wa siasa nchini, jukumu ambalo haliwezi kulikwepa.
“Maridhiano ndani ya chama hayakuanza leo wala jana, historia ya kuanzishwa kwa TANU na ASP, msingi mkuu wa kuliunganisha taifa ulikuwa maridhiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii,” alisema
Alifafanua kuwa, mwaka 1957, chama cha TANU kilibeba jukumu la kuratibu maridhiano wakishauri wenzao upande wa Zanzibar hadi kufanikisha kuzaliwa kwa chama cha ASP baada ya kuungana vyama vya African Association na Shirazi Association.
Shaka alisema mwaka 1961, ASP kiliingia kwenye maridhiano Zanzibar ambapo Sir George alikuwa kiongozi wa Serikali na Hayati Mzee Abeid Amani Karume, alikuwa Waziri wa Afya.
“CCM hatufanyi kazi hiyo ya maridhiano ndani ya Tanzania pekee bali, hata nje ya mipaka. Wakati Zimbabwe inataka unganisha baina ya vyama vya ZANU na ZAP, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alishiki hadi kuzaliwa kwa ZANU-PF.
“Mzee Kinana (Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara) alikuwa mpatanishi Sudani Kusini. Chama kina viongozi ambao ni mahiri wa maridhiano na mashauriano,” alibainisha.
Shaka alinukuu Ibara ya 14 ya ilani ya uchaguzi ya CCM, Ibara 110, Ibara ya 118 na Ibara 120 ambazo zimezungumzia namna Serikali za Chama Cha Mapinduzi zitavyokwenda kusimamia maridhiano.
Akielezea kile kilichojadiliwa katika vikao hivyo baina ya Rais Samia na viongozi wa vyama vya siasa, Shaka alisema muda ukifika Watanzania wataelezwa kile kilichojadiliwa.
Alisisitiza kuwa, Rais Samia na viongozi hao wa vyama vya siasa, wana nia njema yenye maslahi kwa Watanzania.
Na MUSSA YUSUPH, DODOMA