CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewaonya viongozi wa Jumuiya za Chama wanaoanza kupanga safu za uongozi kabla ya uchaguzi mkuu wa Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani, kwani kitawachukulia hatua wote watakaobanika.
Aidha, Baraza Kuu la Umoja wa Wazazi CCM limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha taifa kupata mkopo wenye masharti nafuu wa sh. trilioni 1.3, ambao unatumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akifungua kikao cha baraza hilo kilichofanyika Desemba 22, 2021, jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, alisema mwakani kutakuwa na uchaguzi ndani ya Chama na Jumuiya zake hivyo, haitarajiwi watu wakiuke taratibu.
“Chama kina imani uchaguzi huo utaendeshwa kwa ustaarabu na kanuni za Chama na Jumuiya, lakini uchaguzi huo bado kampeni zake hazijaruhusiwa. Ipo minongíono miongoni mwenu mmeanza kupiga kampeni kinyume na maadili ya Jumuiya zetu,” alisema na kuonya:
“Tunasikia watu wanabeba viongozi na wengine wameshaanza kutoa na kupokea rushwa, hivyo ni vema mkaacha, wala msithubutu kwani hakuna kisichofahamika na Katibu Mkuu wa Chama anafahamu yote.”
MALI ZA CHAMA
Kuhusu mali za Chama, Kanali Lubinga alisema kuna viongozi ambao siyo waadilifu wanahujumu mali za CCM.
Aliwataka viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kuwa waaminifu katika kutenda haki na kuzilinda mali za Chama zikiwemo shule zinazomilikiwa na Jumuiya hiyo.
“Nina wasiwasi kuwa baadhi hatujui historia ya shule zetu za wazazi, shule hizi zimeinua elimu ya Tanzania na zilikuwa na uwezo mkubwa, lakini baadhi ya viongozi wasio waadilifu wamezifilisi na nyingine zimeuzwa, hela hazionekani,” alisema.
“Viwanja vya Chama vimepotea na atakayethubutu kufuatilia kujua ukweli anaonekana ni adui, kama walionunua wangekuwa na tamaa kama hizi zilizopo leo, sisi tungekuta nini, lazima tujiulize maswali hayo ili kila mmoja akawe mlinzi wa mwenzake,” alisisitiza.
PONGEZI KWA RAIS
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Daniel Sayi, alisema baraza hilo limeazimia kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia kwa kuwezesha kupatikana kiasi hicho cha sh. trilioni 1.3.
“Hakuna asiyeonana sasa miundombinu inatekelezwa kwa kasi, ikiwemo barabara, reli ya mwendokasi, zahanati, meli zinatengenezwa na katika sekta ya mazingira,” alisema na kuongeza:
“Tunayo heshima kumpongeza Rais Samia, katika sekta ya elimu zimetengwa shilingi bilioni 368 za kutekeleza miradi mbalimbali katika shule za msingi na sekondari, sasa tunasema jambo la mama ni jambo la Jumuiya ya Wazazi.”
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dk. Edmund Mndolwa, alimpongeza Rais Samia kwa kuteua makatibu wa wilaya 16 kutoka katika Jumuiya hiyo.
Alisema kutokana na Jumuiya hiyo kuwa na mrundikano mkubwa wa madeni, wamejipanga kwa kila fedha wanazopata kutenga asilimia kadhaa kulipa madeni ya watumishi na wastaafu.
“Tunampongeza Rais Samia kwa kuonyesha upendo katika Jumuiya yetu kwa kuteua watendaji 16 kitu ambacho hakijawahi kutokea, hiyo inaonyesha kuwa ana imani na sisi kwa kuthamini mchango wetu,” alisema.
Dk. Mndolwa aliongeza kuwa hadi sasa kikao hicho kimekutanisha wajumbe 96 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Naye, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Dk. Philis Nyimbi, alitaka kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya Jumuiya za Chama ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
“Tuendelee kuimarisha ushirikiano miongoni mwetu, yaani jambo la Jumuiya liwe jambo la Chama, itaongeza ufanisi katika Chama, kuimarisha Jumuiya zetu na kuongeza uwezo wa utendaji kazi kwa mtu mmoja mmoja,” alisema.
Na FRED ALFRED, DODOMA