CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeziagiza halmashauri ambazo hazijatoa vitambusho vya matibabu kwa wazee kuanza kutoa vitambulisho hivyo bure kwa wazee wanaostahiki.
Agizo hilo la Chama limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Christina Mndeme, wakati akizungumza na wanachama wa CCM, Tawi Namba 3, Kijiji cha Bulembo, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera.
“Zipo baadhi ya halmashauri hazijatoa vitambulisho vya wazee. Watoe vitambulisho hivyo mara moja ili wazee wanaostahiki wapate matibabu bure,” alieleza.
Alisema kuna maeneo walipewa vitambulisho wazee wasiostahiki na ndio sababu vikasitishwa matumizi yake kwa baadhi ya halmashauri, lakini sasa vitambulisho hivyo vianze kutolewa kuwawezesha wazee kuendelea kupata matibabu bure.
Kadhalika, aliagiza hospitali zote ziwe na dirisha maalum la dawa kwa wazee na daktari atakayewahudumia na si wapange foleni kusubiri matibabu.
Aliwahakikishia wazee wa tawi hilo kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwahudumia wazee kwa kuhakikisha huduma muhimu za matibabu zinaendelea kupatikana hospitalini.
“Katika mwaka huu wa fedha, Rais wetu Samia ametoa Tsh. bilioni 260 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba hospitalini,” alieleza.
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, aliwaomba wazee kuendelea kusisitiza malezi bora na maadili mema katika jamii hususan kwa vijana.
“Kumetokea mmomonyoko wa maadili kwa vijana, kwenye daladala hawawapishi wakubwa wala hawasalimii. Maadili yakiporomoka ndio chanzo cha kuenea kwa uhalifu,” alisema.
Pia, aliwaagiza mabalozi wa mashina kuweka kipaumbele cha ajenda ya ulinzi na usalama kwenye vikao vyao kwa dhumuni la kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarika kuanzia shina, kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa.
MAKUNDI NDANI YA CHAMA
Akizungumzia kuhusu makundi ndani ya Chama, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara alisema kiongozi mwenye kuendekeza makundi amepoteza sifa ya kuendelea kuwa ndani ya CCM.
“Ogopeni rushwa, makundi na kuchafuana. Wanaoendekeza makundi wamepoteza sifa ya kuwa viongozi kwa sababu makundi hayana afya ndani ya Chama.
Aliongeza kuwa: “Mmeshaanza makundi ya kupanga safu, acheni kabisa. Wazee kemeeni vitendo hivi.”
Mndeme alisema umoja na mshikamano ndio chachu ya ushindi, hivyo viongozi waliopo wanapaswa kuachwa kuendelea kutimiza majukumu yao hadi pale kipyenga cha uchaguzi kitakapopulizwa mwakani.
KADI ZA KIELETRONIKI
Akizungumzia kadi za kieletroniki kwa wanachama, alisema kadi zaidi ya 300,000 zimeshachapishwa na baada ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia, kuzindua kadi hizo zitasambazwa kwa wanachama.
Alitoa rai kwa viongozi wa CCM kuendelea kusajiri wanachama kisha kuwapatia kadi za vitabu wakati wakisubiri kadi mpya za kieletroniki.
Aidha, aliagiza mabalozi wa mashina yote 431 wa Wilaya ya Missenyi kupatiwa bendera na vitabu vipya vya orodha ya wanachama.
“Katiba ya CCM inaeleza kwamba bendera ya CCM itapeperushwa kuanzia kwenye mashina. Katibu wa CCM Wilaya hakikisha mabalozi wote wanapatiwa bendera na kwa wale ambao vitabu vya orodha ya wanachama vimejaa, watapatiwa vitabu vipya,” alisisitiza.
NA MUSSA YUSUPH, MISSENY