SERIKALI kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imetatua changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama iliyodumu kwa miaka 60 katika Kisiwa cha Jibondo, Wilaya Mafia, Mkoa wa Pwani.
Hatua hiyo, inatokana na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliogharimu sh. bilioni 1.9.
Imeelezwa kuwa kutokana na ukosefu wa maji kwa kipindi hicho na kutokuwepo kwa chanzo cha uhakika cha huduma hiyo, serikali iliamua kuipatia ufumbuzi kwa kupitisha mabomba ya maji chini ya bahari umbali wa kilomita saba kutoka Kijiji cha Kiegeani, Kitongoji cha Utende.
Hayo yalielezwa na Meneja wa RUWASA Mafia, Clement Lyoto, baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA, Profesa Idris Mshoro, kutembelea mradi huyo na kufafanua kuwa ujenzi wake ulianza mwaka 2018 na utawanufaisha wakazi 2,050 .
Lyoto alibainisha kuwa ukosefu wa chanzo cha uhakika kilikwamisha kisiwa hicho kupatiwa huduma hiyo, hivyo wakazi wa Jibondo walilazimika kutumia maji yaliyovunwa wakati wa msimu wa mvua.
Aliongeza kwamba ili kukidhi hitaji la maji katika kipindi cha kiangazi, wananchi walilazimika kununua maji kutoka kijiji cha Kiegeani kwa sh. 700 hadi sh. 1,500 na kuyasafirisha kwa kutumia vyombo vya baharini.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Clement Kivegalo, alisema mradi huo mkubwa na wa kujivunia umeleta tija kwa wananchi waliokuwa wakipoteza muda mwingi kusaka maji kwenda na kurudi umbali wa kilomita 20.
Kivegalo alisema eneo hilo lilikuwa halina chanzo cha uhakika cha upatikanaji wa maji, ambapo serikali ilihangaika namna ya kulitatua tatizo hilo na kulazimika kutandaza mabomba ya maji chini ya bahari kilomita saba.
“Huu ni mradi ambao RUWASA tunajivunia na umetupa uzoefu wa kufanya miradi mingine mikubwa yenye changamoto ya aina hii,” alisema.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA, Profesa Mshoro, alihimiza kutunza mradi huo na kuzingatia mapato na matumizi, huku akisema kujenga miradi ni rahisi, lakini tatizo namna ya uendeshaji wake baada ya ujenzi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Maji Jibondo, Halfan Mohammed, alisema skimu inatoa huduma ya maji kwa wakazi wa vitongoji sita vya Kijiji cha Jibondo kwa kupitia vituo vya kuchotea maji vya jamii 20.
Baadhi ya wakazi wa Jibondo akiwemo Sophia Ally, walisema upatikanaji huo wa maji umekuwa mkombozi kwao, hivyo wanaishukuru serikali na RUWASA kwa kumtua ndoo mama kichwani ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Na Mwamvua Mwinyi, Mafia