WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, imepokea msaada wa chanjo ya Uviko-19 aina ya Sinopham kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Akipokea msaada huo katika makabidhiano yaliofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Mjini Zanzibar, Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Simai Mohammed Said, amesema jumla ya chanjo dozi 200,000, zimepokelewa ambazo zitatumika kuchanja wananchi wapatao 100,000.
Amesema hiyo ni awamu ya pili kwa chanjo aina hiyo kutoka Serikali ya China, kuipatia Zanzibar ambapo awamu ya kwanza, ilipokea dozi 110,000 ambazo zilitumika kuchanja wananchi 52,000.
Pia, amesema mapokezi hayo yanafanya kuwa na jumla ya chanjo zilizopokelewa nchini tangu kutolewa dhidi ya Uviko-19 hadi sasa kuwa dozi 422,520.
Amesema jumla ya watu 1,39,431, wamepata chanjo kamili Zanzibar, ambapo kati ya watu waliochanjwa, hakuna taarifa yoyote ya kupata madhara na kuthibitika kuongeza kinga mwilini na kupunguza makali kwa wale waliopata maambukizi ya virusi vya korona.
Hata hivyo, amesema kwa sasa, takwimu zinaonyesha mkoa unaofanya vizuri katika kutekeleza utoaji wa chanjo ya Uviko- 19 ni Mkoa wa Mjini Magharibi, hivyo jitihada zaidi zinahitajika kwa mikoa mengine.
Naye Balozi Mdogo wa China nchini, Zhang Zhi Sheng, amesema Serikali yake itaendeleza mashirikiano zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuchukua jitihada za kupambana na uviko 19 nchini.
Aidha, amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa mapambano dhidi ya Uviko- 19.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Dk. Fatma Mrisho, ameshukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada wake kwa Zanzibar.
Aidha, amewataka wananchi kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na Uviko 19 ikiwa ni pamoja na uvaajia barakoa, kunawa mikono kwa maji na sabuni kwa kutumia vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa na lazima.
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMED , ZANZIBAR