ZIKIWA zimebaki siku mbili kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu wa Chama, Daniel Chongolo, amesema malengo ya sasa ya Chama ni kuongeza uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Chongolo ameyasema hayo katika kipindi maalumu kinachorushwa na Kituo cha runinga cha Channel Ten, jijini Dar es Salaam na kueleza kwamba, alipopewa nafasi hiyo, Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, alimuagiza kujielekeza katika kuongeza uwezo wa kujitegemea.
Alisema majukumu mengine aliyokabidhiwa ni kuhakikisha anaboresha maslahi ya watumishi ndani ya Chama, kujenga mifumo itakayoendelea kukiimarisha Chama na yote hayo yamefanyika.
Kuhusu kujitegemea, alibainisha kuwa, tayari wamekamilisha kazi ya utambuzi wa mali zote cha Chama.
“Tumeangalia tuna mali gani, ziko wapi, zitatusaidia katika nini na hatua ya pili ni kuzitumia mali zile kwenda katika kuongeza tija na uwezo wa kujitegemea kama taasisi, hilo tunalifanya na tunakwenda vizuri sana,” alisema.
Aidha, Chongolo alitaja jambo linalomkera zaidi ni baadhi ya watu kushindwa kutimiza wajibu wao.
“Mtu anapewa jukumu hasimami vizuri, anashindwa kwa hiyo, mnalazimika kumsubiri awafikie mlipo ndiyo muendelee, anachelewesha inakera sisi vijana tunatamani mambo yaende haraka kwa kasi,” alisema.
Alieleza kuwa, mambo mengi yanayoonekana kero ndiyo siasa yenyewe, hivyo yanavumilika, yanatatulika kwa kutumia akili.
Alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiamini CCM, kwani nia yake ni kutekeleza ahadi zote ilizozitoa katika Ilani yake ya uchaguzi, waendelee kuamini kwamba, dhamana iliyonayo CCM lazima kuitekeleza usiku na mchana.
Alibainisha kuwa, sekta mbalimbali za huduma, zimeboreshwa zikiwemo elimu, afya na maji.
Alieleza kuhusu maana ya alama za jembe na nyundo katika bendera ya CCM, zinamaanisha kwamba, Chama ni cha mkulima na mfanyakazi.
“Wengine wanasema mbona kuna wafanyabiashara, wafanyabiashara na mkulima wote wanafanya biashara, huwezi kulima na kuacha shambani, utaenda kwenye soko, hapo tayari utakuwa mfanyabiashara,” alisema.
Hata hivyo, alifafanua kuwa, chama cha CCM hakijawahi kubadili, haitabadili wala haifikirii kubadili itikadi yake, kwa sababu msingi kinachoendana nao ni wa ujamaa na kujitegemea.
“Msingi ulioasisi chama chetu ni ujamaa na kujitegemea, sisi ni wajamaa kweli kweli ambao tunaamini katika kujitegemea, hili neno kujitegemea ndugu zetu Wachina wao ni wajamaa na ujamaa una misingi inayoujenga lakini Wamarekani ni mabepari na hawaogopi kujiita hivyo.
“Wenzetu juzi walikuwa wanahangaika na sera ya afya bure kwa wote huo sio ubepari, maana ubepari ni aliyenacho awe nacho asiye nacho atajua mwenyewe lakini ujamaa ni kilichopo tugawane wote,” alisema.
Kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, kinatarajiwa kufanyika kitaifa wilayani Musoma, Mkoa wa Mara.
CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya muungano wa vyama vya ASP na TANU vilivyotumika kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ambayo sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
NA JUMA ISSIHAKA