KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ametoboa siri ya CCM kuendelea kudumu madarakani kwa kipindi cha miaka 45, kuwa ni mifumo imara inayoendeleza imani kwa wananchi na kujikosoa miongoni mwa wanachama.
Ametaja siri nyingine ni kutokana na utekelezaji wa matakwa ya wananchi na mabadiliko ya kimfumo.
Katibu Mkuu huyo, ameyasema hayo Januari 31, 2022, alipozungumza katika kipindi maalumu cha kuelekeza miaka 45 ya CCM kinachorushwa na kituo cha Channel ten.
Chongolo amesema siri ya CCM kuendelea kuaminiwa ni hatua yake ya kutekeleza yale ambayo wananchi wanahitaji na Chama kubadilika kutokana na wakati na mazingira.
“Tumekuwa na awamu za kufanyia mapitio ya sera, mifumo na namna tunavyojiendesha sisi kwa sisi ndani, tunakosoana tena kabisa, mfumo huo uliratibiwa na Baba wa Taifa kutengeneza mazingira ya sisi kwa sisi kukosoana,” amesema.
Amefafanua kwamba iwapo CCM kitajijengea mazingira magumu ya kuendeleza imani ya wananchi, ni wazi upinzani utaimarika na wananchi kuhamisha imani zao huko.
“Kwanza ni mfumo wa ndani, udhaifu wa wapinzani unajengwa na mfumo na uimara wao unajengwa na mfumo huo huo, sisi tukijitengenea mazingira magumu ya kuendeleza imani ya wananchi kwetu, wale kule (wapinzani) wataimarika.
“Sababu imani itahamia kwao, lakini kile kinachofanyika ndani kwanza. Mfumo wetu unakumbuka mwaka 1982 tulitengeneza mfumo wa kujikosoa sisi kwa sisi ndani kwa ndani,” amesema.
Akizungumzia asili ya jina la Chama Cha Mapinduzi, Chongolo amebainisha kwamba wakati huo Chama kilianzishwa kwa lengo la kuleta mapinduzi ya ukombozi wa mataifa hususan wa mtu mweusi.
“Kwanza tulianza na ukombozi wa Tanzania na tulipomaliza tulianza na wenzetu, tumehangaika na Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Namibia, Botswana, Afrika Kusini na mataifa mengine,” amesema.
Ameeleza kuhangaika huko kulihitaji uwepo wa mapambano na Tanzania ndiyo iliyokuwa kitovu cha kuendesha mapinduzi na mageuzi ya kimfumo kutoka kutawaliwa na wakoloni hadi kujitawala, hilo ndilo chimbuko la jina Chama Cha Mapinduzi.
Kauli hiyo ya Chongolo inakuja zikiwa zimebaki siku chache kuelekea maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM, yatakayofanyika kitaifa wilayani Musoma Mkoa wa Mara, Februari 5, mwaka huu.
CCM ilizaliwa Februari 5, mwaka 1977 baada ya muungano wa vyama vya ASP na TANU vilivyotumika kupigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ambayo sasa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Juma Issihaka