KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ametoa wito kwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kuhakikisha zinaanzisha ujenzi wa Chuo Kikuu Pemba ili kurahisha upatikanaji wa elimu.
Chongolo alitoa wito huo, akiwa Pemba katika ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 na kuhimiza uhai wa chama ngazi ya mashina.
“Sasa ni wakati wa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu hapa Pemba, ili vijana wanapomaliza elimu ya sekondari iwe rahisi kujiunga na Chuo Kikuu moja kwa moja, na wengine kutoka maeneo mengine waje kusoma na kujifunza hapa Pemba,” alisema.
Chongolo alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za mafunzo ya ujuzi yanayotolewa katika vyuo vya kati, ili kuendana na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya madarasa, hospitali, vituo vya afya na barabara.
“Vijana mkajifunze ujuzi. Ujuzi ndio msingi wa maendeleo ya kila mmoja wetu, ujuzi wa ufundi ni muhimu, kwani serikali inatoa fedha nyingi kwa ajiili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali na fedha zote hizo ni muhimu mkazipata ninyi hapa mkiwa na ujuzi.
Chongolo alitoa maelekezo hayo, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahoro Matrar, ambapo mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imepanga kujenga vyumba vya madarasa 215, matundu ya vyoo 500, hospitali za wilaya katika wila zote za mkoa huo na ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 75.
Alisema ujenzi wa miundombinu yote hiyo unahitaji vijana wenye mafunzo ya ufundi ambapo SMZ inatoa bure kwa vijana wote wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla.
Aidha, Chongolo akiwa katika mkutano wa shina namba 5 Tawi la Mtambile jimbo la Mtambile, alieleza umuhimu wa sensa ya watu na makazi, ambapo amesisitiza mipango ya maendeleo inayopangwa na serikali, hutegemea idadi ya watu katika eneo husika.
Wakati huo huo, Chongolo alitoa wito kwa wanchama wa CCM katika uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, kuchagua viongozi wenye uchungu na maendeleo ya watu na wanaohangaika na changamoto za watu na sio watu wanaokaa kusubiri fursa ndani ya Chama.
“Ninyi hapa mnajuana ni nani anafaa kuwaongoza kwa namna anavyoishi na nyie na namna anavyohangaika na shida zenu usiku na mchana, hao ndio muwashawishi wagombee nafasi za uongozi,”alisema Chongolo.
Chongolo alitembelea na kukagua shughuli za shirika la Bandari Pemba na baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Bandari Pemba, Abdulah Salim Abdulah aliridhishwa na utendaji.
Na MWANDISHI WETU, PEMBA